KUREJEA kwa kiungo mkabaji, Mkongomani Mukoko Tonombe kumelipa ugumu benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Mtunisia Nasreddine Nabi na msaidizi wake Mrundi, Cedric Kaze.
Tonombe hajacheza mechi yoyote ya kimashindano ya Yanga msimu huu, akitumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu baada ya kumpiga kiwiko mshambuliaji wa Simba, John Bocco kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), Julai 25, mwaka huu.
Kiungo huyo mwenye hamasa katika timu hiyo akiwa uwanjani, Jumatatu aliungana na wachezaji wenzake kambini katika kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC FC utakaopigwa Uwanja wa Majimaji, Songea.
Mmoja wa mabosi wa Benchi la Ufundi la Yanga, ameliambia Championi Ijumaa kuwa kurejea kwa kiungo huyo kumemfanya kocha Nabi apate ugumu wa kupanga kikosi chake cha kwanza.
Bosi huyo alisema kuwa ugumu huo anaupata kutokana na muunganiko mzuri ulikuopo kati ya viungo wawili wakongwe Khalid Aucho na Yannick Bangala ambao wamecheza michezo iliyopita na kufanya vizuri.
Aliongeza kuwa kwa viwango ambavyo wamevionyesha katika mchezo wa Ngao ya Jamii na miwili ya ligi dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold, Nabi ameonekana kupata ugumu baada ya Tonombe kurejea kikosini.
“Kwa usajili bora uliofanywa na viongozi, kocha anakabiliwa na changamoto ya upangaji wa kikosi chake kutokana na ubora wa kila mchezaji.
“Ugumu umeongezeka zaidi ni baada ya kurejea kwa Tonombe ambaye alikuwa nje ya uwanja katika michezo mitatu akitumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu baada ya kumpiga kiwiko Bocco.
“Tonombe anarejea uwanjani lakini tayari wapo viungo Aucho na Bangala ambao wameonekana kucheza vizuri kwa kuelewana kwa ubora mkubwa, hivyo kazi kubwa anayo Nabi,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo, Kaze alisema: “Kikubwa tuna kikosi bora na imara cha kupata matokeo mazuri, hilo ndilo jambo la kujipongeza,ushindani wa namba msimu huu ni mkubwa kutokana na ubora wa kila mchezaji. Ni kipindi chetu hivi sasa benchi la ufundi kutulia na kuandaa kikosi kitakachotupa pointi hilo ni jambo la muhimu zaidi," .
Mukoko kiwango kimeshuka
ReplyDelete