WAKATI timu zinaenda kwenye mapumziko mafupi kupisha mechi zilizopo kwenye Kalenda ya FIFA, Manchester United haikuwa katika ubora wake hasa baada ya sare na vipigo vya hapa na pale ikiwa imecheza mechi kumi za michuano yote msimu huu.
Matumaini ni kuona Premier League inaporejea, Kocha Ole Gunnar Solskjaer anakuja na mbinu mpya na ile hadhi ya Man United inarudi tena.
Heshima hiyo inarudi kwa kushuhudia timu ikicheza kwa kiwango na kuona Man United inakuwa na staili yake ya kucheza kwani kwa misimu ya karibuni imekuwa ikicheza soka, lakini halijulikani ni la aina gani, yote kwa yote mashabiki wanataka kuona timu inashinda na kutwaa mataji msimu huu.
Ndani ya Pisi Kali ya Man United, leo nataka kutoa pongezi kwa mastaa wetu wawili, Cristiano Ronaldo na Marcus Rashford ‘New Doctor in Town’, hawa wiki hii wameipaisha timu yetu ya Manchester United kwa rekodi nzuri.
Ronaldo yeye wiki hii alifanikiwa kuibuka kuwa mchezaji bora wa mwezi Septemba wa Premier League.
Staa wetu huyo katika mwezi Septemba alicheza dhidi ya Newcastle United, West Ham United na Aston Villa, akifunga mabao matatu katika mechi hizo.
Lakini pia Ronaldo alishindanishwa na wachezaji kama Mohamed Salah (Liverpool), Joao Cancelo (Manchester City), Antonio Rudiger (Chelsea), Allan Saint-Maximin (Newcastle United) na Ismaïla Sarr (Watford) kuwania tuzo hiyo.
Ronaldo aliwafunika wote na kupata tuzo hiyo ambayo kupata sio jambo rahisi na hii ni kutokana na ushindani ambao upo ndani ya Premier League.
Ikumbukwe kuwa Ronaldo aliondoka mwaka 2008 ndani ya Man United na Premier League kwa ujumla akijiunga na Real Madrid ambao alianza nao kazi msimu wa 2009/10.
Amerudi nyumbani sasa na kuendeleza pale alipoishia kwani wakati anaondoka mwaka 2008, mwezi Machi aliibuka kuwa mchezaji bora ndani ya Premier, hivyo kupata kwake tuzo ndani ya ligi hiyo ni kama mwendelezo wa pale alipoishia miaka 12 iliyopita.
Hivyo, Ronaldo anastahili pongezi kwani licha ya kuwa na miaka 36, bado uimara wake umeendelea kuonekana ndani ya uwanja.
Ni wazi kuwa staa huyo amekuja kuendeleza alipoishia kwani ndani ya Premier anahistoria za kuchukua tuzo za namna hiyo za mwezi na zile za mchezaji bora wa msimu.
Kasi ambayo ameanza nayo Ronaldo basi ihamie kwa wengi pia kama ambavyo Bruno Fernandes naye alivyotisha mwaka 2020 akitwaa tuzo za Premier League za mwezi mara nne.
Ukiachana na tuzo ya Ronaldo, zao la Akademi ya Man United, Rashford wiki hii alipewa udaktari wa heshima na Chuo Kikuu cha Manchester kutokana na kazi kubwa ambayo alifanya kwa jamii.
Kwa sasa anafahamika kama Daktari Marcus Rashford MBE na ameweka rekodi kwani ni mchezaji mdogo zaidi kupewa heshima katika historia ya Chuo Kikuu cha Manchester.
Rashford mbali na kupambana uwanjani, ila alifanya kazi kubwa kipindi cha janga la virusi vya corona lilipoibuka kwa kuwasaidia watoto ambao walikuwa wanaishi katika mazingira magumu kwa kuwapata chakula hasa mashuleni na hata kuishauri serikali kutoa msaada jambo ambalo ni ngumu kwa kijana wa aina yake.
Lakini kama haitoshi baada ya kujitoa huko Rashford, Malkia wa Uingereza alimpongeza mchezaji huyo na kumuita kwenye kasri lake ikiwa ni heshima kubwa kwa kiasi kikubwa kwa mchezaji huyo.
Rashford amepata heshima hiyo, lakini huko nyuma ndani ya Man United heshima ya namna hiyo walipata wakongwe wa timu yetu kama Sir Alex Ferguson na Sir Bobby na hii inaonyesha jinsi gani Man United tunavyorithishana vitu vizuri.
Makala haya yanapatikana katika gazeti la Spoti Xtra
0 COMMENTS:
Post a Comment