January 31, 2014


 Na Maulid Kitenge
KOCHA wa Simba Mcroatia, Logarusic wiki iliyopita alifanya kitu ambacho kilimshangaza kila mmoja wakati Simba ilipokuwa inacheza na Rhino Rangers ya Tabora kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Kitendo hicho ni kile cha kumuingiza dakika kama ya 86 hivi kwa mshambuliaji Betram Mwombeki na kisha na kumtoa dakika chache tu baada ya kumuingiza.

Imewashangaza watu kiasi mpaka kitendo hicho kulaaniwa na Chama cha Wanasona Tanzania (Sputanza).

Kimewashangaza watu kwa vile haijueleweka kosa la Mwombeki ni nini mpaka alimuingiaza na kumtoa dakika chache. Kitendo hicho kilionekana kumuuzunisha Mwombeki kiasi cha wachezaji wenzake kumpoza baada ya mechi.

Logarusic kwa mtazamo naona ni mwalimu ambaye anacheza sana na jukwaa na kutafuta sifa zaidi na hii ni hatari sana kwake. Aombe Mungu mambo yaende vizuri lakini siku yakibadilika ni hao hao mashabiki watakaombadilikia.

Ukiangalia amekuwa na mbwembwe nyingi zisizo za maana kabisa kwa Kocha makini hapaswi kuwa hivyo hata kidogo. Kitendo cha kubadili tu mchezaji anavyojisikia, kucheza na jukwaa na maneno mengi yasiyokwisha ipo siku yatamtokea puani. Lakini kwa vile mambo sasa yanakwenda vizuri hakuna anayeona hili. 

Kitu kingine ambacho kilinistaajabisha kwa kocha huyu Mcroatia ni kitendo wakati mchezaji wake Ramadhani Singano akipiga penalti katika mechi hiyo yeye kugeukia kwa mashabiki akiwa hataki kuangalia.

Hivi najiuliza ataonaje makosa ya mchezaji wake kama Kocha na wewe unaogopa kuangalia penalti ya mchezaji wako? Hii ilinishangaza kweli.

Logarusic anachofanya yeye ni zaidi ya shabiki sasa. Hivi juzi tumesikia ameingia katika bifu na beki wake Joseph Owino kiasi cha kumpeleka kikosi cha pili. Anaonekana anafanya ukali pasipokuhitajika ukali.

Nakubaliana naye katika suala la nidhamu lakini sio katika ukali anoufanya na kucheza na jukwaa hasa katika mechi. Ndiyo maana nasema wakati huu mambo yanaenda vizuri mashabiki utakuwa nao mgongoni lakini mambo yakibadilika, utabaki mwenyewe Logarusic.

Punguza mbwembwe zisizo na maana na jaribu kufanya mambo kama kocha unayejiamini na upunguze maneno, maana watu wangependa kuona Simba inacheza soka ya kueleweka kwa kuwa na Kocha wa kigeni sio mbwembwe zisizo na maana. Ni hilo tu.

Kuna mengi yanaweza kujitokeza, kuna sehemu Logarusic anaweza akawa sahihi, lakini suala la kukosea pia linamgusa kutokana na matendo anayofanya.
Mpira ni mchezo wa makosa, haiwezekani kila akikosea mchezaji, basi anakwenda benchi, lazima kuwe na utaratibu ambao unatambulika.

Kweli Logarusic ni mtaalamu, lakini anatakiwa kujua uongozi unahusisha mambo mengi ikiwemo molari pamoja upendo. Lazima ajue, muhimu kuonyesha upendo na kukosoa kwa lengo la kufundisha si kukatisha tamaa au kuharibu.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic