Na Saleh Ally
WAKATI mwingine nimekuwa najiuliza mambo maswali mengi sana
kuhusiana na suala la ubaguzi wa rangi ambalo linaonekana wakati mwingine
kulielemea Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Nianze na mkasa wa juzi ambao umemtokea kiungo nyota wa Brazil,
Ronaldinho Gaucho ambaye hivi karibuni amejiunga na klabu ya Querétaro ya
nchini Mexico ambako anaamini ndiyo atamalizia mpira wake.
Ronaldinho amebaguliwa, amedharauliwa na kuitwa sokwe, licha ya
kwamba hakuwa na kosa hata punde.
Aliyembagua ni mwanasiasa maarufu wa chama kinachojulikana kama
National Action Party (Pan) ambaye pia amewahi kuwa waziri wa serikari ya
Mexico.
Jamaa anaitwa Carlos Manuel Treviño ambaye ameingia kwenye kundi
la wapuuzi na wajinga wanaoamini ubaguzi wa rangi ni nyenzo.
Kisa cha kumbagua Ronaldinho ni kwa kuwa mwanasiasa huyo alikuwa
akitokea katika mihangaiko yake anarejea nyumbani, kukawa na foleni kubwa sana
njiani na mwisho aligundua inatokana na mashabiki wa klabu ya Queretaro waliokuwa
wakitokea kwenye Uwanja wa Corregidora kumpokea kiungo huyo alipokuwa
anatambulishwa.
Akaamua kuweka maneno ya kashfa kwenye mtandao wa kijamii wa
Facebook akimuita sokwe ambaye amesababisha yeye kuchelewa kufika nyumbani.
Mpira ni burudani kubwa lakini ni chombo bora kabisa cha
kuwaunganisha watu mbalimbali wakiwemo wale waliogombana, wasiopendana au
kutoelewana.
Nchi nyingi zilizoingia kwenye vita hasa vile vya wenyewe kwa
wenyewe, mwisho zimetumia nguvu zaidi kwenye mchezo wa soka ili kurejesha hali
ya utulivu.
Mfano mzuri ni Wanyarwanda ambao baada ya mauaji ya kimbari
mwaka 1994, soka ndiyo chombo kilichosaidia kwa asilimia kubwa kuwaunganisha,
pia kujitahidi kusahau mabaya na makali yaliyopita.
Sasa jiulize, wakati wengine wanatumia soka kama chombo
unganishi, vipi hao wanatumia mchezo huo kama chombo tenganishi kwa lengo la
kudharau, kuonea au kubeza bila hata sababu yoyote ya msingi.
Ninazungumzia Wazungu, ninazungumzia watu weupe wanaoamini ni
bora kuliko Weusi hata kama heshima yao haiko juu kama wanavyofikiri.
Wakati mwingine unaweza kufikiri hata wao Fifa ni wababaishaji
kwenye hili kwa kuwa hakuna adhabu kali zaidi kwa wanaofanya hivyo viwanjani.
Kuna kila sababu ya kuliangalia zaidi kwa kuwa wale wanaowabagua
weusi, wanakuwa hawana heshima ya kimatendo au hata fedha dhidi yao.
Angalia waliombagua Samuel Eto’o au Yaya Toure kule Urusi. Mfano
mwingine wale mashabiki ambao huwabagua wachezaji Waingereza au kule Hispania.
Ajabu hili linafanywa hata na wachezaji kwa wachezaji, nafikiri
ndiyo ungekuwa mfano mzuri zaidi kuwaonya wabaguzi wengine.
Ikitokea mchezaji kambagua mwenzake, halafu ushahidi ukawa
umepatikana kwa uhakika, basi afungiwe msimu mzima.
Wale mashabiki wanaweza kujifunza kupitia adhabu kali ambazo
watapata wachezaji, makocha, viongozi na hata waamuzi ambao wataonyesha
ubaguzi.
Nani kasema ngozi nyeupe au ngozi ya mzungu ndiyo akili? Upuuzi
mtupu!
Tunajua Fifa ina Wazungu wengi kuliko Weusi, huenda linaonekana
si suala kubwa sana na mapambano yake yako kwenye mapango tu bila ya vitendo.
Huenda adhabu ingekuwa kali sana kama Waafrika wangekuwa na
nafasi ya kuwabagua Wazungu pia. Fifa bado inahusika na inapaswa kujua upole
wake katika hilo, unazidi kufanya liendelee.
Wazungu wanaobagua Weusi ni wapuuzi, Fifa haipaswi kuacha upuuzi
huo uendelee kwa kuwa si Weupe tu ndiyo wanaoujua kuucheza mpira na mfano mzuri
wa kuwa Weusi wanaujua mpira, jikumbushe kwa Pele.
Wajinga kama mwanasiasa yule wa Mexico aliyembagua Ronaldinho
ambaye sasa tayari yuko katika hali mbaya kisiasa kutokana na kusakamwa sana na
mashabiki wa soka, wanapaswa wapate joto ya jiwe kama anayokutana nayo, la
sivyo hawataacha.
Lakini kwa Fifa na mashirikisho ya soka Ulaya, nayo yapambane
kuzuia hilo kwa kuwa inakuwa ajabu, hata Wazungu wenye njaa, nao wanawadharau
Waafrika wenye mafanikio zaidi eti kisa ni Weupe. Huu ni upuuzi mkubwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment