March 1, 2013




MILOVAN AKIONDOKA DAR JUZI USIKU...

*Afunguka kila kitu kuhusu usajili, awataja adui wa Simba

Na Saleh Ally
BAADA ya maneno mengi, hatimaye aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amebeba mabegi yake na kurejea kwao Serbia akiwa rasmi ameachana na mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Milovan ndiye aliyewapa Simba ubingwa, dalili zinaonyesha msimu huu si wao. Ameondoka baada ya kulipwa fedha zake na Mlezi wa Simba, Rahma Al Kharusi ‘Malkia wa Nyuki’ ambaye alijitolea kulimaliza tatizo hilo.

Milovan, baba wa watoto watatu, Sarah, Ana na Malta, alikuwa anaidai Simba mishahara minne, jumla ni dola 32,000 (Sh milioni 51.8), ingawa Malkia wa Nyuki alimlipa dola 35,000 ili amalize na matatizo yake mengine kama hoteli na tiketi ya ndege.

Jumatano saa nane na nusu usiku, wakati Milovan akiwa njiani kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Championi Ijumaa lilifanya mahojiano naye ambayo yalikuwa ya mwisho akiwa katika ardhi ya Tanzania.

Milovan anaeleza mambo kadhaa kuhusiana na hali ilivyo huku akisisitiza kuna viongozi na wadau wa Simba ambao wamekuwa wakifanya juhudi kumchafua, kitu anachoamini si sahihi kwa kuwa yeye hakuwa adui wa Simba, badala yake wao ndiyo tatizo kubwa.

“Lengo langu si kumshambulia mtu, lakini nakuhakikishia Simba haitatulia, kuna matatizo mengi na viongozi ndiyo chanzo. Leo ninazungumza hapa, lakini baadaye nitakaa kimya na kuacha ukweli uonekane, baada ya muda utaonekana tu.

“Hapa mwisho, nilifanya kazi katika mazingira magumu sana Simba, uongozi uliachia matundu mengi, ikawa rahisi kila mtu kuingia na kuzungumza anachotaka au kukufundisha bila kujali wewe ni kocha,” anasema Milovan na kuendelea kuelezea mambo kadhaa.

Vijana:
Mimi ndiye nilikuwa wa kwanza kuchukua uamuzi wa kuwapa wachezaji makinda nafasi, nakumbuka nilikutana na upinzani mkali, ilionekana hawataweza. Lakini nilishikilia msimamo, ninashukuru vijana hawakuniangusha, walicheza vizuri.

Baadaye, siku ninapoamua kuwaweka benchi kutokana na ninavyoiona mechi ilivyo mbele yetu, utashangaa kiongozi analaumu eti siwapangi, tena anakasirika kabisa. Lakini kiongozi huyu ndiye alikasirika sana baada ya mimi kuanza kuwapa nafasi hadi kufikia kusema ninawaharibia timu.

Wenye fedha:
Wenye fedha ni muhimu sana katika klabu au uhamasishaji wa timu, lakini baadaye waligeuka na kuwa tatizo. Kuna huyu jamaa anayependa kuvaa kofia kubwa, awali nilijua ni mtu mzuri sana.

Lakini alinishangaza sana, kila mechi alianza kunifundisha wakati wa mapumziko. Alitaka nipange wachezaji kwa mfumo wake. Kweli hiyo ilinishangaza sana, nimeisomea chuoni kazi hii kwa miaka kumi na moja.

Jiulize, mtu ambaye anaona tu pale uwanjani au kwa kuwa mara nyingi anakwenda uwanjani, anaamini anajua kuliko wewe. Bora angeshauri na si kukufundisha au kuamrisha, niligundua tatizo moja, kwamba kwa kuwa wana fedha, basi wanaamini wanajua kila kitu. Hilo ni tatizo kubwa sana la Simba.

Kaseja hatarini:
Watu haohao wenye fedha ndiyo wamekuwa wanaharibu mambo mengi, mfano kushinikiza mchezaji acheze wakati kocha unamuona hajawa tayari na inapotokea akashindwa kufanya vizuri, wanageuka na kukuangushia lawama.
Ninaamini, subiri muda utaeleza kila kitu.
(Juma) Kaseja ambaye mimi ninaamini ni kipa bora kabisa atakumbana na hali hiyo. Watafikia kushinikiza kipa mgeni (Abel Dhaira) acheze, lakini likitokea tatizo, watamuangushia mzigo mwingine kabisa, hilo ni tatizo jingine kubwa.

Ochieng & Akuffor:
Nilisikia kuna kiongozi mmoja alikuwa akijitahidi kunichafua kwenye mitandao na vyombo vya habari, mimi nimefanya kazi ya mpira siku nyingi. Najua nifanye nini, nimesomea hii kazi, siwezi kuwa kama yeye, ndiyo maana hata jina simtaji, ninajua ninachofanya.

Wanasema mimi niliwasajili kina Daniel Akuffor na Paschal Ochieng, hiki ni kichekesho kwangu, eti nimeitia Simba hasara, kwa lipi? Niliporudi nikawakuta, wakaniambia niwaangalie tukiwa Arusha, nikafanya hivyo na kutoa majibu.

Wale wachezaji si wabaya, nasisitiza si wabaya na wana uwezo. Lakini inaonekana walikokuwa hawakuwa wakicheza au vinginevyo, walihitaji muda. Niliwaambia ni wachezaji wazuri ambao wanahitaji muda, wao walitaka siku mbili wawe wazuri, kitu ambacho hakiwezekani.

Leo matatizo yao, mwisho wakaniangushia mimi ndiye nilisema wasajiliwe. Mchezaji pekee niliyempendekeza asajiliwe wakati huo ni (Mrisho) Ngassa, wao hili wanalijua.

Yondani:
Angalia Kelvin (Yondani), aliondoka wakati tunamhitaji, Simba leo inahangaika sana kwa sababu yake. Ndiye beki bora wa kati Tanzania, hakuna timu anayoweza kwenda akakosa namba. Anaijua kazi yake, yupo makini na hana utani hata sekunde moja.

Waliniambia wamemuongezea mkataba, nilisisitiza kuhusiana na umuhimu wake. Sikutaka kusema moja kwa moja, ila nilianza kuhofia ataondoka baada ya kusikia haelewani na kiongozi mmoja ambaye kila siku anakorofishana na wachezaji.

Nikaona bora nisisitize kuhusu kuongezewa mkataba, wakaniambia kila kitu tayari, nikiwa Serbia nikasikia amejiunga Yanga, sikuamini.

Tatizo hilo Simba watakaa nalo kwa muda mrefu, limewatia hasara kubwa mara kumi zaidi ya fedha ambazo wangetoa kumbakiza Kelvin. Ndiyo maana nasema wanaamini wanajua mambo, kumbe hapana.

Boban & Nyosso:
Niliingia kwenye matatizo kuhusiana nao, waliniita tuwajadili katika kipindi ambacho tayari wamewasimamisha, lakini siku ya mwisho wakasema walinishirikisha, hakikuwa kitu sahihi. Niliposema likawa kosa la jinai.

Hawa ni watu wa ajabu kabisa, Milovan akikosea walitaka apambane na makosa yake, lakini wakikosea wao, wanataka watu wote waingie kwenye makosa hayo. Ajabu sana!

Mafisango:
Mimi sikuangalia sana mambo binafsi kama wanavyofanya wao, nilitaka kazi yangu iende kwa mafanikio. Kama unakumbuka marehemu Mafisango alinitukana, lakini nilisisitiza abaki, maana tulikuwa tunamhitaji sana Sudan, hapa niliangalia maslahi ya Simba na Milovan.

Lakini Boban alisimamishwa kwa kuwa alizozana na mtu mmoja si kiongozi, lakini huwa ni mtu wa karibu wa Simba na anayetoa msaada. Akasimamishwa, mimi sikuona sawa kwa kuwa nilikuwa namhitaji, msaada wake ulikuwa muhimu kwa wakati huo.

Angalia hao watu wenye fedha wanavyopenda heshima, ukiuliza yeye ni nani hadi Boban anasimamishwa, haupati jibu. Lakini siku ya mwisho wanasisitiza tulishiriki wote, pia nilipohoji nikaonekana ni adui. Wangekuwa wazalendo kwa Simba, wangeangalia maslahi ya timu kama nilivyofanya kwa Mafisango.

Hata iwe vipi, lazima viongozi na watu wa karibu wa Simba wakubali, kama wanampa kocha kazi, basi wamuache afundishe na kufanya kazi yake kwa ufasaha, wasiingilie anachokifanya, wasimshinikize, huo si weledi.

Kuna mengi nimeyaona Simba, lakini wao ndiyo wananifanya niseme leo kwa kuwa wanadanganya umma. Nilichoamua nikifika Serbia, nitapumzika, nitaacha kuzungumzia Simba ili angalau niisahau kwa kuwa inaniumiza ninapoikumbuka. Lakini wakizidi kunisakama, nitamtaja mmoja baada ya mwingine na madhambi yao.

SOURCE: CHAMPIONI SPORTS NEWSPAPER..

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic