Kuna ujumbe
mfupi wa maneno umeenezwa kwenye baadhi ya simu za mkononi za wapenzi wa Simba
zikidai kwamba washabiki wa Yanga waliokuwa wakiishangilia klabu yetu jana
walifanya hivyo kwa sababu klabu hizi mbili zimeingia katika mahusiano.
Ujumbe huo
ukadai kwamba lengo la mahusiano hayo mapya baina ya Simba na Yanga ni
kuhakikisha kwamba Simba inafungwa kwa idadi kubwa ya mabao kwenye mechi ya
watani wa jadi Mei 18 mwaka huu.
Ujumbe huo,
ukaenda mbali zaidi kwa kudai kwamba hata kambi ya Simba ya Bamba Beach
imefadhiliwa na Yanga.
Ujumbe huo
wa simu ni wa kuchekesha. Na unachekesha sana. Yeyote aliyetunga meseji hii ana
nia ya kuleta machafuko ndani ya klabu ya Simba. Inaonekana haridhishwi na hali
ya amani iliyopo klabuni kwa sasa.
Uongozi wa
Simba unakana kuwepo kwa mahusiano yoyote ya kuhujumu timu baina ya viongozi wa
klabu na Yanga. Kitendo cha kushangiliwa kwa timu pinzani si kigeni kwani
kimewahi pia kutokea katika nchi kadhaa duniani.
Ikumbukwe
kwamba kimsingi, si jinai au mwiko kwa shabiki wa Yanga kuishangilia Simba.
Kama washabiki wa wapinzani wetu wa jadi walivutiwa na kiwango chetu na kuamua
kutushangilia, hiyo haikuwa dhambi.
Uongozi
unapenda kuwaomba wanachama wa Simba kuwa na imani na uongozi wao na kufahamu
kwamba unafanya kila unaloweza kulinda na kuhifadhi hadhi na heshima ya klabu.








0 COMMENTS:
Post a Comment