*Ni mtoto wa kiongozi wa zamani wa Simba
Na Saleh Ally
SOKA la England lina mashabiki wengi duniani kote, Tanzania ni moja ya sehemu ambayo mchezo wa soka na ligi hiyo vinapendwa sana.
Manchester United ni kati ya timu maarufu zaidi na zenye wapenzi wengi hadi Tanzania. Lakini ni nadra kusikia shabiki amefunga safari au yumo katika Uwanja wa Old Trafford unaomilikiwa na klabu hiyo akishuhudia mchezo wowote wa timu hiyo.
Mohammed Jawad Kassam ambaye ni mwafunzi wa Chuo Kikuu cha Brunel cha jijini London, alikuwa mmoja wa Watanzania wachache walioshuhudia mchezo wa Ligi Kuu England kati ya wenyeji Manchester United na Swansea na mechi ikaisha kwa United kushinda kwa mabao 2-1.
Kwa Kassam, kitu kikubwa hakikuwa kuiona mechi hiyo, lakini kuwa katika Uwanja wa Old Trafford katika siku muhimu ambayo haitatokea tena katika historia ya klabu hiyo.
Kocha Mkuu, Alex Ferguson alikuwa anaangwa, ndiye anaamini kuwa kocha mwenye mafanikio zaidi kuliko wote duniani katika ngazi ya klabu.
Ferguson aliyeipa Man United makombe 13 ya Ligi Kuu England, aliwaaga mashabiki kwenye uwanja huo, lakini karibu dunia nzima ilishuhudia mechi hiyo muhimu na ya kihistoria.
Moja ya vitu alivyovifanya Kassam ni kuinua bango aliloliandika hivi “Thank you Sir Alex, with love from Tanzania”. Kwamba “Nashukuru sana Sir Alex, kwa mapenzi kutoka Tanzania”.
Bango hilo la Kassam ambaye baba yake Fazal Kassam aliwahi kuwa mweka hazina wa klabu ya Simba, lilizua gumzo kubwa katika mitandao. Inagwa wako walionekana kutopenda yeye kupongezwa, lakini wengi wlaifurahia na kusema wazi walitamani kuipata nafasi hiyo muhimu zaidi.
Championi: Hongera kwa nafasi hiyo, vipi ulifanikiwa kupata tiketi hiyo?
Kassam: Nashukuru, tuna kundi letu la marafiki ambao baadhi yao ni Watanzania na Wakenya, wao wanaishi hapa Uingereza. Wao ni Season Ticket Holders (wana ticketi za mwaka mzima kwenda Old Trafford game zote). Ndio nikanunua tiketi kutoka mmoja wao kwa bei ya pauni 50.
Upatikanaji wa tiketi kwa mechi kama hizi ni ngumu sana kwa kweli, tiketi ziliuzwa dola 5000 kwenye intaneti na uwanjani ziliuzwa hadi dola 1000 (Sh milioni 1.6), dakika za mwisho. Nawashkuru sana marafiki zangu kwa bei waliyonipa kupata tiketi hiyo.
Salehjembe: Hiyo ni mara yako ya kwanza Old Trafford?
Kassam: Tangu nilipokuwa mdogo, nilikuwa na ndoto ya kwenda OT, siku moja na kukukutana na angalau Ferguson. Tangu nimekuja huku kusoma mwaka 2011, nishawahi kufika kama mara nane hivi, ikiwemo katika mechi dhidi ya Liverpool na ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Madrid
Salehjembe: Hali ilikuwaje njiani wakati wa kwenda uwanjani?
Kassam: Kuanzia asubuhi, redio, runinga, kwenye mitandao yote ishu ilikuwa ni mechi hiyo ya Ferguson kuaga. Tukiwa njiani tulipishana na gari nyingi zenye bendera za Manchester United. Kusema kweli, Tanzania tuko mbele zaidi kwenye kushangilia hasa tunapokuwa tunakwenda uwanjani katika mechi.
Wao naona wametuzidi wanapokuwa wameingia uwanjani, maana hapa, njiani huwa huoni fujo sana, lakini ukikaribia uwanjani na mziunguko ya uwanjani, unasikia nyimbo tofauti tofauti zikiimbwa. Tofauti moja kubwa ambalo ninapenda sana sie Watanzania tuifanyie kazi ni jinsi ya ushangiliaji katika viwanja vya huku. Wanaimba nyimbo za aina tofauti, watu wanashangilia mwanzo mwisho na pia huwa watulivu na wenye heshima sana.
Salehjembe: Ulipoingia uwanjani, nini ulikiona ni tofauti ukilinganisha na hapa nyumbani?
Kassam: Kila kiti kilikuwa na bendera ya Champions 20, ila mie sikuchukua bendera bali nika onyesha bango langu, ndipo watu walipogeuka na kunishangaa, wengine wakichukua picha na kunipigia makofi. Na kuanzia pale ndipo watu wa runinga, wapigapicha walikaribia kwangu na kuchukua picha.
Salehjembe: Kulikuwa na Watanzania wengine?
Kassam: Niliowaona mimi ni wawili, pamoja na mimi, Wakenya walikuwa wanne na hili ndilo kundi tulikwenda pamoja uwanjani. Ila pale uwanjani niliketi karibu na mtu kutoka Urusi na wengine kutoka Hispania, Waingereza na wengine ambao sikuweza kutambua uraia wao.
Salehjembe: Vipi hukupata hata bahati ya kumsogelea Ferguson?
Kassam: Uwanjani nilikuwa karibu na Ferguson, tukiwa na umbali wa viti kama 10 hivi kushoto kwangu. Tuliruhusiwa kusimama na kuchukua sahihi yake, ila nilichelewa kwa sababu tulikutana na foleni ndefu. Ila baada ya kuchukua kikombe, alipita karibu nasi kabisa nikamuona kwa karibu.
Salehjembe: Ilikuwaje kwa mashabiki baada ya hotuba yake?
Kassam: Baadhi ya watu walimwaga machozi waliposikia hotuba ya Ferguson. Kwa kweli, kuna wengi waliokuwa na huzuni kuona Ferguson akistaafu.
Salehjembe: Kama unapenda soka, hapa nyumbani ni shabiki wa timu ipi?
Kassam: Nyumbani Tanzania ni shabiki kubwa sana wa Simba Sports Club, huwa nakwenda nda mara nyingi sana uwanjani, pia kuna wachezaji wa Simba ni rafiki zangu. Nakukumbusha pia, Simba iko katika familia yetu maana baba yangu mzazi, Fazal Kassam alikuwa mweka hazina wa Simba enzi hizo kipa alikuwa ni Mohammed Mwameja.
0 COMMENTS:
Post a Comment