Na Saleh
Ally
WAKATI
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Osmund Mbilinyi alipokuwa akichangia makadirio ya
bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo bungeni, kuna mambo
kadhaa aligusia kuhusiana na wasanii.
Mbiliyingi
maarufu kama Sugu kwa watu wa sanaa, alikuwa mkali katika mambo kadhaa na
ilionyesha wazi alilenga kuwasaidia wasanii ambao wamekuwa wakitesema kutokana
na jasho lao kwenda mikononi mwa wajanja wachache.
Pamoja na
kuonyesha nia ya dhati, Sugu alizungumza maneno mawili ambayo yalibaki
yakizunguka kichwani mwangu na kunikumbusha mambo mengi niliyopitia katika
harakati ambazo Sugu ameziendeleza bila ya kuchoka.
Katika
changia hiyo, Sugu alisema wasanii wengi ni waoga, waache unafiki na kutetea
maslahi yao, kitu cha pili akasisitiza suala la umoja kwamba hakuna umoja kati
yao.
Wakati
anasisitiza umoja, alisisitiza kwa kusema: “Anachokililia Lady Jaydee leo
ndicho Vinega walikuwa wanakipigania miaka yote. Wakati fulani ilifikia watu
wakasema tunahongwa ili kufanya hivyo, lakini kikubwa kwetu ilikuwa ni kudai
haki zetu.”
Kuna watu
wengi sana duniani, kama ilivyo kwa wasanii lakini mara kadhaa ili kukamilika
kuwa msanii, kuweza kupiga gitaa na kuimba pekee hakutoshi hata kidogo.
Suala la
kutetea haki zako ni muhimu, lakini kwa kuwa msanii anaingia katika kundi la
wasanii, lazima kuwe na umoja ili kulifanya kundi hilo liwe na nguvu na kuweza
kupambana kama timu na kama ni vita, basi washinde pamoja.
Vita ya
wasanii imekuwa ni sawa na mapambano ya walishika mitutu ya bunduki, wengine
wakiwa wamejaza matenga ya nyanya ambazo wanazitumia kama risasi kuwaponda
wengine ili kutaka kupata haki zao.
Wasanii
wengi ni wanafiki, wabinafsi kupita kiasi na siku zote wamekuwa wakiifanya vita
ya wasanii dhidi ya wanaolalamikiwa iwe laini sana kwa kuwa wengi wao
hawafanani kati ya sura na mioyo yao.
Jiulize,
wasanii wangapi wanaweza kusimama na kumtetea mwingine hata tatizo
linalozungumziwa halimhusu yeye, angalau amesikia mwenzake ana tatizo. Asilimia
kubwa wamekuwa wakifurahia matatizo ya wasanii wenzao.
Kufeli kwa
msanii mmoja ni faraja kwa msanii mwingine, hiyo inakuwa inatoka moyoni, lakini
kama wakitulia, usoni wanaonekana tofauti na kusisitiza kwamba wanataka haki za
wasanii.
Nimesema
mara kadhaa, wasanii wengi hawatetei haki za wasanii hadi wanapoguswa na
kusikia uchungu. Wengi wao ‘wananunulika’ kwa ulahisi sana. Naweza kusema hivi,
wenye uchungu na fani yao ni wachache kuliko wasaliti.
Ndiyo maana
nayachukua maneno haya mawili ya Sugu, unafiki na wasio na umoja. Ninasema hivi
kwa kuwa nina ushahidi, nakumbuka mwaka 2003, nilishiriki katika kampeni za
kusaidia kuunda umoja wa wasanii zilizokuwa zinaongozwa na Innocent Nganyagwa
na Mr II au 2 Proud.
Wakati huo
nilijifunza mambo mengi sana ya wasanii, pamoja na kuandaliwa mikutano kadhaa,
lakini karibu kila mkutano ulikuwa haufikishi zaidi ya wasanii nane wakati
waliokuwa wanaahidi kuja kwa midomo yao walikuwa zaidi ya 40.
Mwisho
Nganyagwa na 2 Proud mnayemuita Sugu sasa, wakakata tamaa na kuamua kuendelea
na hamsini zao. Lakini siku chache kati ya wasanii ambao walikuwa hawaonekani
katika vikao hivyo, akalaumu kwenye vyombo vya habari kwamba wasanii hawana
ushirikiano.
Nimejifunza
mengi sana katika kuripoti kwangu kuhusiana na muziki, nilianza kuripoti muziki
tokea mwaka 1996 nikiwa shuleni. Tokea wakati huo katika gazeti la Msanii
Afrika, ninachokiona mbele yangu ni nguo yenye matobo ambayo wasanii wanajaribu
kuitumia kujifunika kuepuka baridi.
Haitawezekana
hata siku moja kwa kwa mmoja mmoja. Ushirikiano ndiyo ungewawezesha wasanii
kuwa na nguvu ya pamoja na kuweza kupambana. Lakini kinachotokea ni wasaliti
ndani ya chumba cha mapambano dhidi ya maadui.
Unafiki
ndiyo sifa kubwa ya wasanii wengi wa Tanzania, wakiwemo wale wanaotaka kuficha
sura zao kwenye sura ya uungwana na kuidanya jamii, eti wanaonewa na wao
wanapewa sapoti kubwa sana kwa jamii.
Wanasema
hivyo kwa kuwa wameumizwa wao, hawajajali vipi sanaa wanayoitumikia imeumia.
Kibaya zaidi, walishindwa kuitetea sanaa ilivyoumia, wakiumia wao, wanataka iwe
vita ya sanaa yote kuwatete,a kitu ambacho nakiona ni upuuzi mkubwa.
Sitaki
kuwataja kwa majina, ila nawakumbusha wasanii kibao ambao mliwahi kusema Sugu
ameisha ndiyo maana anapiga kelele tu. Leo mnaomuona shujaa na kutafuta urafiki
tena, mbaya zaidi katika umri mdogo mlionao, albamu na nyimbo chache na hata
umaarufu wa siku chache, nyie ndiyo mmeisha kabisa!
Wasanii mnapaswa
kujiangalia upya, wanapaswa kutafuta rekodi na kutathimini upya kwamba bado
haitoshi kujificha katika kivuli cha Sugu ambaye amekwenda katika njia yake,
hata waliomchukia na kumsema vibaya leo wamerudi upande wake.
Hebu
jaribuni angalau wasanii kumi tu kuwa wakweli na wapambanaji kama Sugu muone
kama hakutakuwa na mabadiliko. Sisemi muwe maadui wa adui zenu, ikiwa hivyo
hakutakuwa na mafanikio katika mnachokitaka.
Ninachosisitiza,
mpambane kwa ajili ya maslahi ya sanaa yenu ambayo itakuwa ndiyo mafanikio yenu
na mabadiliko yatapatikana.
Lakini
nisisitize, mnakosea sana kupendana machoni na mioyo yenu imejaa roho ya kutu,
hamtaki maendeleo ya wenzenu mkiwa mmesahau kuwa kama kuna mtu anaendelea,
maana yake anakupa changamoto na wewe kujipanga na kufikiria kupambana ndiyo
njia sahihi ya kuleta maendeleo.
Mnataka
wengi wawe waoga, wasio na uwezo wa kupambana na kufanikiwa. Lakini ajabu,
mnataka tasnia ya muziki iwe imara na inayoheshimika. Kwa kuwa ninawajua,
kwangu nawaona sawa na paka anayewinda samaki wa mapambo aliye ndani ya kioo,
akiamini atamkamata na kupunguza njaa yake.
NINAAMINI, WASANII NDIYO JAMII INAYOSIKILIZWA ZAIDI NA JAMII, HIVYO MKIUNDA UMOJA WA DHATI KILA KITU CHENU KITASIKIKA KWA ULAHISI ZAIDI, LAKINI MKIENDELEA NA UNAFIKI KAMA ILIVYO SASA. MTAENDELEA KULALAMA HADI MWISHO WA DUNIA.
makala nzuri sanaa tenaa sanaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa uwiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii wasanii wengi nuwanafiki na waoga wanapambana leo na kujidai wapo na sugu sababu hawana tena pakukimbilia makala ninzuri uwiiiiiiiiiiiiiiiii nzurii sanaaa
ReplyDelete