Na Saleh Ally
Niliwaona mashabiki kadhaa wa timu ya
taifa kutoka upande wa jukwaa la Yanga wakizomea kwa juhudi kubwa wakati
wachezaji wa Taifa Stars wakitoka uwanjani kwenda vyumbani.
Wachezaji hao walikuwa wanaingia
vyumbani vichwa chini mara baada ya kupata kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wageni
wao Uganda ‘The Cranes’ katika mechi hiyo muhimu sana.
Mechi hiyo ya kuwania kucheza fainali za
Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (Chan) nchini Afrika Kusini
ilichezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na matarajio ya
wengi, nikiwemo mimi ilikuwa ni kuiona Stars ikiibuka na ushindi.
Nilitamani sana kuiona Stars ikishinda
mechi hiyo, lakini bado niliamini hata baada ya ushindi majibu sahihi
yangepatikana katika mechi ya marudiano mjini Kampala wakati Uganda itakapokuwa
nyumbani.
Kufungwa kwa Stars kumeonyesha
kuwakatisha tamaa watu wengi waliokwenda uwanjani hasa kwa kuwa walikuwa na
matumaini makubwa na kikosi cha Stars chini ya Kim Poulsen ambacho kimekuwa
kikionyesha soka la uhakika.
Ndiyo maana wengine wakaona uamuzi
sahihi ni kuwazomea wachezaji hao, kwangu naona hapana na hata kama walituudhi
Watanzania, sidhani kama ni sahihi kuwashambulia wanajeshi wako wakati wakiwa vitani.
Ikumbukwe kwamba Stars ilitakiwa icheze
mechi mbili, moja ni hiyo ambayo imechezwa Dar es Salaam, halafu ipo ya pili
mjini Kampala ambayo Uganda watakuwa wenyeji.
Stars wamepoteza wakiwa wenyeji, mimi
ninaamini hata Uganda wanaweza kupoteza, lakini kama wachezaji wa Stars, benchi
la ufundi na wanaowaandaa wataamini hivyo.
Majibu ya kama Stars imefuzu au la
hayajapatikana, kuwashambulia sasa si sahihi na si ushabiki unaolenga kujenga
na kusaidia. Hadi wachezaji hao wanajenga imani kubwa kwa mashabiki maana yake
walifanya kazi vizuri.
Kuwazomea wakati wana jukumu mbele, la
kulitetea taifa letu ni sawa na kujishambulia sisi wenyewe kwa kuwa tunazidi
kuwavunja nguvu hata kabla mapambano hayajafikia tamati. Sikubaliani na
waliojishambulia kama Watanzania, naona wana haraka.
Bado niko katika kundi la kuamini soka
ndiyo mchezo wenye matokeo yasiyotabirika kirahisi na Stars bado ina nafasi ya
kusonga mbele, hasa kama itaamua kwa dhati.
Kwa sasa mjadala ni Stars itafanya nini
kushinda mechi ijayo na ikiwezekana kusonga mbele, lakini pia kujiuliza iliteleza
wapi katika mechi ya juzi hadi kushindwa kuonyesha kiwango chao kilichozoeleka,
kiasi cha kufungwa bao 1-0 dhidi ya Uganda.
Baada ya hapo, kocha Poulsen na cwachezaji
wake wakae na kuyafanyia kazi matatizo ambayo yalikuwa chanzo cha wao kushindwa
katika mechi hiyo na kuyapatia majibu. Wafanye mazoezi vizuri halafu
wakapambane ugenini na inawezekana kabisa wakashinda na kusonga mbele.
Hadi sasa Stars wako nusu ya safari na bado
njia ya wao kwenda Chan haijafungwa kwa kuwa wana dakika 90 muhimu mbele yao na
zinawezekana kutumika kuipeleka Tanzania Afrika Kusini na hilo ni jukumu lao
kama wawakilishi wa nchi.
Waliowazomea ni Watanzania wenye uchungu
na nchi yao, inawezekana walishindwa kuzuia hasira zao. Wao hawapaswi kuweka
hayo akilini mwao kama hoja ya msingi, badala yake nini kifanyike katika mechi
ya pili ili Stars isonge hadi Afrika Kusini ndiyo jambo la msingi zaidi na hoja
nzito.
Binafsi bado ninaamini Stars bado ina
nafasi ya kufuzu, kikubwa ni kurekebisha makosa na kufanya maandalizi ya
kutosha na hasa kujifunza kupitia mechi ya kwanza. Lakini kisaikolojia, ni
kuamini kuwa kuishinda Uganda kwao inawezekana na Stars inaweza kwenda Afrika
Kusini.
Fin.







0 COMMENTS:
Post a Comment