Saleh Ally
Inawezekana wengi wanaweza wakawa
wanajiuliza namna ambavyo mshambuliaji Luis Suarez Alberto anavyogombewa.
Suarez anagombewa katika kipindi akiwa
na matukio lukuki yanayoonekana kumpeleka katika dimbwi la wachezaji watukutu
ambao hakika unaweza kusema hawana nidhamu.
Inakuwaje kama UIaya na kwingineko
kulikoendelea kisoka wanasisitiza sana suala la nidhamu halafu kipindi hiki
wanamgombea Suarez ambaye nidhamu yake inaonekana hakuna lolote?
Ana matukio mengi ya utovu wa nidhamu kama
kuwauma wenzake, akianzia wakati akiwa Uholanzi akiichezea Ajax, lakini
akarudia baada ya kumuuma beki Branislav Ivanovic wa Chelsea katika moja ya
mechi za Premiership.
Lakini kabla ya hapo, Suarez alihusishwa
na matukio kibao likiwemo lile la kuushika mpira kwa makusudi wakati wa mechi
ya Kombe la Dunia wakati Uruguay ilipokuwa inaivaa Ghana.
Kwa mfano wa Suarez inaonyesha kiasi
gani Wazungu wanavyoangalia utendaji kwanza, halafu suala la nidhamu linafuatia
baada ya hapo.
Wanachoangalia kwa Suarez ni uwezo
zaidi, ndiyo maana Arsenal na Real Madrid zimekuwa zikichuana vikali kumpata
mshambuliaji huyo Mruguay huku Liverpool ikionyesha kufanya juhudi za kutaka
kumbakiza.
Siku chache baada ya Suarez kumuuma
Ivanovic, Liverpool ilimpa adhabu lakini ikasisitiza kuendelea kubaki naye na
kuweka katika mtandao wake ujumbe uliokuwa unasema hivi: “Suarez si mtu mwenye
matatizo na kama analo tatizo ni kwa kuwa hapendi kushindwa, hupenda kufanya
lolote ili ashinde.”
HAKUNA KUREMBA:
Timu zote tatu zina kila sababu ya
kuchanganyikiwa na utendaji wa Suarez, kwanza ni kati ya wachezaji wachache
wanaoonyesha uwezo wa kujituma kwa nguvu sana.
Suarez anacheza tofauti na wachezaji
wengi maarufu, wachambuzi wa soka wanamlinganisha na Lionel Messi ambaye
hucheza kwa juhudi muda wote na kutaka kushinda.
Angalia anavyocheza Suarez, hakika
hakuna ‘kuremba’ na hucheza kwa kujituma mwanzo mwisho.
MGUSA NYAVU:
Alijiunga na Liverpool, Januari 2011
akiwa ametoka kutikisa katika Kombe la Dunia lililofanyika nchini Afrika
Kusini.
Suarez alikuwa ameonyesha kuwa yeye ni
mchezaji tofauti katika Kombe la Dunia, lakini kabla ya hapo rekodi yake ya
ufungaji akiwa na Ajax katika Ligi ya Uholanzi ilikuwa juu.
Katika msimu huo wa 2009-10, aliweka
rekodi ya kufunga mabao 49 katika mechi 48. Ilikuwa kubwa na ambayo inaweza
kumuweka mchezaji katika kiwango cha kuitwa “World Class Player”.
PASI ZA MABAO:
Ukiachana na suala la kipaji chake cha
kufunga mabao na uwezo mkubwa wa kujituma, Suarez ana kitu cha ziada ambacho
timu nyingi sana zinahitaji, pasi zinazozaa mabao.
Mchezaji ambaye anafunga na kutoa pasi
zinazozaa mabao kwa wingi ni lulu katika nchi zilizoendelea kisoka.
Suarez alimaliza muda wake katika Ligi
ya Uholanzi akiwa amecheza mechi 159 na kufunga mabao 111. Pia alitoa pasi 37
zilizozaa mabao kwa timu yake na Liverpool hawakuwa na ujanja zaidi ya
kumchukua.
MASHUTI:
Suarez anazidi kuwa lulu kwa kuwa katika
msimu ulioisha wa Ligi Kuu England, alikuwa kati ya wachezaji wanaowania nafasi
ya kuwa mchezaji bora lakini akaharibu mwisho kwa kumuuma Ivanovic.
Pamoja na kuwa na uwezo wa mambo mengi,
wastani wa 4.2 wa kupiga mashuti yaliyolenga langoni ulimfanya ashike nafasi ya
tatu baada ya Robin van Persie wa Man United aliyekuwa na 4.4 na kinara Wayne
Rooney aliyemaliza na 4.7.
Hii ni sehemu ya kuonyesha kwamba Suarez
anatosha kuwa mchezaji wa kuwaniwa na timu nyingi kubwa za Ulaya na kila moja
inatamani kumpata kwa kuwa ni msaada.
Hadi ligi hiyo ya England maarufu kama
Premiership inamalizika, Suarez pia alishika nafasi ya tatu kwa kufunga akiwa
na mabao 16, Rooney 17 na kinara van Persie 25.
MAISHA:
Inawezekana Wazungu ni wepesi
kuchunguza, wameona Suarez aliyezaliwa miaka 26 iliyopita katika Mji wa Salto
nchini Uruguay, alikulia katika mazingira magumu hasa baada ya wazazi wake
kutengana akiwa na miaka tisa, ikiwa ni miaka miwili tu baada ya kuhamia katika
Jiji la Montevideo.
Wanajua wafanye nini kupata alichonacho
kama msaada au faida na vigumu kukipata kwa wengine. Suarez amemuoa mpenzi wake
wa siku nyingi aitwaye Sofia Balbi na wamezaa mtoto aitwaye Delfina na
inaelezwa maisha katika familia yake yamejaa amani na hakuna utukutu kama
anaofanya uwanjani.











0 COMMENTS:
Post a Comment