Na Saleh Ally
Mwaka 2010 wakati wa Kombe la Dunia nchini Afrika
Kusini, mtaalamu wa masuala ya penalti, Ignacio Palacios-Huerta, alipewa kazi
na timu ya taifa ya Uholanzi kuchambua upigaji penalti wa Wahispania.
Palacios-Huerta ni profesa katika chuo cha
masuala ya uchumi jijini London, England. Alipewa kazi hiyo kwa kuwa tangu
mwaka 1995 alikuwa amejisomea na kuchambua penalti 9,000.
Baada ya Hispania na Uholanzi kuingia fainali,
alianza kuifanya kazi hiyo kwa saa 48. Na alitoa majibu kadhaa kama vile “Fernando
Torres kawaida hupiga chini na sababu zake, Xavi na Andrés Iniesta hupiga kulia
kwa kipa na sababu zake na mambo mengi zaidi.” Lakini bahati mbaya timu hizo
hazikufika kwenye penalti baada ya Iniesta kufunga bao pekee la mchezo huo.
Ukiachana na kazi hiyo aliyopewa Profesa
Palacios-Huerta, hadi leo timu ya taifa inayoongoza kufanya kazi na vyuo vikuu
katika mechi zake ni Ujerumani.
Chuo Kikuu cha Sporthochschule Cologne ambacho
kinaaminika ndiyo chuo kikuu bora cha michezo duniani, kimekuwa kinashirikiana
kazi zake na benchi la ufundi la timu ya taifa ya Ujerumani.
Maprofesa na wanafunzi wa chuo hicho wamekuwa
wakiandaa ripoti ya kila mechi ambayo inahusu uchezaji wa wachezaji wa timu
hiyo, namna wanavyoshambulia na kulinda.
Mfano, katika fainali ya Euro 2012, Ujerumani
waliteleza kufuata maelekezo ya namna wanavyolinda katika mechi dhidi ya
Hispania na wakapoteza mchezo kwa mabao 2-1.
Walielezwa namna mabeki wao walivyowapa nafasi ya
hadi mita 8 Hispania kupita katikati na katika mchezo mwingine wakarudia kosa,
wakaadhibiwa.
Kocha mwenye mafanikio zaidi England, Alex
Ferguson, amekuwa akifanya mkutano na wasomi wa Chuo Kikuu cha Manchester mara
mbili karibu kila mwaka ili kujua vitu zaidi.
Amekuwa akikutana na wale wanaosoma biashara na
michezo na hii imemsaidia kuwa kocha bora.
Hii ni mifano michache ya kuonyesha mchezo wa
soka unapiga hatua kubwa tofauti na hapa nyumbani.
Hivi karibuni Simba walianza kuonyesha mfano baada
ya kuwalipa maprofesa wa Chuo Kikuu Huria (OUT), wanaoongozwa na Profesa Tolly
Mbwette kuandaa mpango mkakati wa kuendesha klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 10
ijayo.
Simba wamelipa Sh milioni 15 kwa maprofesa hao,
huenda kwa muda huu wakaonekana kuwa hawafanyi lolote ila mafanikio yakawa
makubwa hapo baadaye.
Pamoja na juhudi hizo za Simba, suala la kufanya
kazi na wataalamu zaidi bado halipewi nafasi, lakini ipo haja ya soka nchini
kuangalia mbali zaidi.
Wachezaji wengi hawana takwimu zao za mechi
walizocheza lakini ajabu zaidi hata klabu hazijui lolote kuhusiana na takwimu
za wachezaji ambazo zingeweza kuwa msaada kwa benchi la ufundi, pia historia ya
klabu.
Soka la kitaalamu linazidi kutuacha mbali sana
kama hata takwimu tu za wachezaji kwa kila mechi klabu hazina. Ipo haja ya
kuajiri wataalamu watakaokuwa wakifanya kazi hizo.
TFF wana wataalamu wao, lakini inaonekana
wamekuwa na majukumu mengi zaidi kuliko hata yaliyowapeleka hapo.
Kutumia takwimu kama mchezaji alicheza vipi mechi
iliyopita, wiki moja na mwezi mmoja uliopita, ni jambo la msingi sana katika
kupiga hatua.
Kwenda kwa kupapasa ni tatizo, lakini kupiga
hatua mbele bila ya kuwa na uhakika wa ulichokifanya nyuma pia ni tatizo
jingine, tena kubwa.
Iko haja leo wataalamu zaidi waaminiwe katika
soka, tena wasiwe wale wataalamu waganga wa kienyeji ambao wamekuwa wakichukua
bajeti kubwa katika klabu.
Ukubwa wa klabu hautoshi kwa jina pekee, soka
linapiga hatua. Kuwa na makocha bora pekee bado haitoshi, lazima tusome alama
za nyakati, hii ni kwa wachezaji na viongozi pia.








0 COMMENTS:
Post a Comment