Lazima kuna tatizo, wachezaji au kocha
wawe wazi ili tubadili gia
Inaumiza sana baada ya kushuhudia kwenye
runinga kikosi chetu cha Taifa Stars kikilambiswa mchanga na Waganda tena
safari hii kwa mabao 3-1, kweli sikuamini.
Nasema hivyo kwa kuwa kuna maswali mengi
sana yanakosa majibu kama utatulia na kujiuliza huku ukiwa umeondoa ushabiki au
mawazo ya kupendelea upande fulani.
Ulimwengu na Samatta:
Akili yangu imekataa kabisa kukubali
kwamba imefikia Taifa Stars haiwezi kufanya vizuri bila ya kuwa na
washambuliaji Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta.
Kumbuka Stars iliwahi kuwafunga Zambia ambao walikuwa mabingwa Afrika bila ya Samatta na Ulimwengu. Hata kama ilikuwa mechi ya kirafiki lakini Zambia hawakuwa na utani maana walikuwa wanakwenda mashindanoni.
Sawa, ukiachana na mechi hiyo ya Zambia, inaonekana hali imekuwa
ngumu katika mechi ambazo Stars imecheza bila ya watu hao, tukianza na ile ya
kwanza ya kuwania kucheza Chan ambayo Stars ililala tena kwa bao 1-0 licha ya
kuwa nyumbani.
Kweli Stars kama ikiwakosa wawili hao basi ndiyo iwe imepoteza mwelekeo, nafikiri si sahihi na kama hilo ni sehemu ya tatizo, basi lazima lipate ufumbuzi mara moja ili kuepuka kuwa na kikosi tegemezi kisichoweza kujitanua kwa nafasi zaidi bila ya kujali yupi hayupo.
Timbe & Micho:
Bado mawazo yangu yanakinzana na hakuna
jibu sahihi zaidi kuhusiana na kukubali eti kwa kuwa Militun ‘Sredojevich
‘Micho’ ambaye ni Kocha Mkuu wa The Cranes na msaizidi wake, Sam Timbe waliwahi
kufundisha soka nchini, basi ndiyo maana Stars imetolewa kinyonge na kwa
kuonewa kiasi hicho.
Maandalizi mabovu:
Hata hili haliniingii akilini, kwamba
kama utasema Taifa Stars ilishindwa kupata maandalizi bora ndiyo maana ikakwama
na kufanya vibaya na Uganda. Tuliona mechi ya kwanza maandalizi yalikuwa mazuri
tukafungwa jijini Dar.
Mechi ya pili, mapema kwa siku 10, timu
ikasafiri na kuweka kambi Mwanza ambako kwa hali ya hewa ni kama Kampala kwa
asilimia kubwa. Tukaona wachezaji wakijifua na kila kitu kilionekana kipo safi
chini ya TFF na wadhamini wao Kilimanjaro.
Sasa ndiyo nafikia kujiuliza tatizo ni
nini kwa kikosi cha Stars ambacho tayari kilijenga imani kubwa kutokana na
kuonyesha uwezo wa juu, kugeuka kwua nyanya kwa timu ya Waganda, tena ile
inayokosa wachezaji wa kulipwa.
Kama wangesema kuongeza wachezaji wa
kulipwa, basi wao wanao zaidi ya 11 wanaocheza nje ya Uganda na huenda katika
wote waliocheza mechi dhidi yetu wasingecheza. Lakini sisi kikosi chetu tunao
wawili tu ambao ni Samatta na Ulimwengu.
Maana yangu hapa ni hivi, kimahesabu sisi
ndiyo tuliopaswa kuwa na kikosi imara zaidi kuliko wao kwa kuwa tumekuwa
tukikitumia hiki hata katika michuano mingine mikubwa chini ya Caf au Fifa.
Sasa vipi wanakuja kutunyanyasa kiasi
hiki? Ndiyo maana nasema kuna kila sababu kama kuna tatizo, basi likawekwa wazi
na kila kitu kikaelezewa wazi kuliko kuficha mambo.
Huu ndiyo wakati mwafaka wa kubadili
gia, mashabiki au wadau kwanza watangulize uzalendo kwa ajili ya kulisaidia
Taifa kujikwamua hapa lilipo kisoma kwa kuwa kama tutacheza kidogo, basi huenda
tukapotea kabisa milele.
Uganda hawakustahili kutushinda, tena
kwa kutunyanyasa kwa kutufunga nyumbani na ugenini, nasisitiza kama TFF wanaona
inawezekana basi watumie muda huu kutafakari mengi na kama ni tatizo wachezaji
au benchi la ufundi basi wafanye mabadiliko mara moja.
Lakini ikionekana kulikuwa na uzembe
ambao umetokea kwenye uongozi mfano TFF, basi wawepo watakaokuwa tayari
kuwajibika ili mambo yabadilike.
Huenda tukasema mambo mengi sana kama
tunalazimika kuwapa nafasi vijana sasa, au tujitoe katika michuano yote na
kuanza kuunda timu upya na vinginevto, kumbe sababu inaweza kuwa ndogo na iko
ndani ya timu.
Kikubwa cha kufanya ni kila upande
ujitadhmini, kama kuna upungufu basi uwekwe wazi na kuanza kufanyika kwa
marekebisho. Mfano, niliwaona wachezaji wa Stars wakicheza kwa kiwango cha
chini na hata morali ilikuwa chini, kuna tatizo miongoni mwao, au hawana
uelewano mzuri na TFF au kuna tatizo jingine basi waseme.
TFF au benchi la ufundi, kama kuna
tatizo au wameshindwa pia wawe wazi. Huu si wakati tena wa kuficha uchi kwa
kuwa hatutafanikiwa kuzaa. Stars imekwama na mambo ambayo yanaweza kutatulika,
hivyo walio ndani au karibu na timu waseme ili tulisaidie taifa letu badala ya
kuacha watu wabahatishe tu.
Kuelezana ukweli kumekuwa kukionekana ni
kama tatizo miongoni mwetu, lakini hatuna ujanja, hatuwezi kukwepa kwa kuwa
ukweli ni dawa hasa bila ya kupendelea au kujali kuna mtu anakasirika. Lakini
bado hatuwezi kupeana dawa ya ukweli kama walio karibu au ndani ya timu
hawatasema tatizo lililowasibu lilikuwa ni lipi.
0 COMMENTS:
Post a Comment