Na Mwandishi wetu,Mwanza
Wadhamini wa timu ya Taifa (Taifa Stars) Kilimanjaro
Premium Lager, wamesema wana imani Stars itafanya vizuri katika mechi ya
marudiano na Uganda Cranes kuwania kucheza katika mashindano ya CHAN kwani maandalizi
ni mazuri.
Hayo yalisemwa na Meneja wa Kampuni ya Bia Tanzania
Kanda ya Ziwa, Malaki Sitaki wakati TBL Mwanza iliwaandalia chakula
cha jioni wachezaji wa Stars.
Aliishukuru TFF kwa kuichagua Mwanza tena iwe Kambi ya
timu ya Taifa kwani wakaazi wa Mwanza wanaipenda timu yao na wamekuwa
wakijitokeza kwa wingi kuangalia wachezaji wakiendelea na mazoezi chini ya
Kocha Kim Poulsen.
“Tuna imani mutafanya vizuri ili twende Chan kama
Waganda walitufunga bao moja kwetu sisi tuna uwezo wa kuwafunga mawili kwao,”
alisema Malaki.
Alisema
kocha amefanya kazi nzuri tangu aanze kuifundisha Timu ya Taifa na anastahili
pongezi kwa mafanikio aliyopata mpaka sasa.
“Matunda mojawapo tuliyoona ni kuwafunga vigogo kama
Zambia, Cameroon na Morocco,” alisema na kuongeza kuwa Kilimanjaro Premium
Lager iko pamoja na Stars kwani ushirikiano uliopo ni wa manufaa kwa pande
zote.
Naye, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba,
aliipongeza Kilimanjaro Premium Lager kwa kuwa karibu na Taifa Stars wakati
wote.
Alisema matokeo ya awali ya Stars kufungwa bao moja
yasiwakatishe wachezaji na wananchi tama kwani kilichotokea ni matokeo ya mpira
na Stars wanaweza kugeuza meza wakiwa Kampala.
Alisema Stars ilivyopiga kambi Mwanza mwaka jana kabla
ya kwenda kwenye mashindano ya CECAFA ilishinda mechi tatu mfululizo kwa hivyo
wanaamini safari hii pia kutakuwa na matokeo mazuri Kampala Jumamosi Julai 27,
Stars itakapocheza na Cranes katika mechi ya marudiano.
Alisema wachezaji wanahitaji sapoti kubwa wakiwa
Kampala na ni muhimu watanzania wanaoishi Mwanza na mikoa mingine ya jirani na
Uganda wajitokeze kwa wingi katika mechi hiyo.
Naye kocha Kim Poulsen alisema wachezaji wako katika
hali nzuri na ana imani watafanya kazi nzuri Kampala.
“Hali ya hewa ya Mwanza ni sawa kabisa na Kampala na
wachzaji wameshazoea na wako katika hali nzuri ya mchezo,” alisema.








0 COMMENTS:
Post a Comment