Klabu ya
Yanga ilipokea barua ya TFF ya tarehe 16/08/2013 kuijulisha adhabu iliyotolewa
kwa Mchezaji Mrisho Ngasa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.
Barua hiyo
inataja adhabu hiyo kuwa nikumfungia Mchezaji Ngasa mechi zipatazo 6 na adhabu
ya kulipa sh. 30milioni pamoja na riba ya asilimia 50% yaani 15milioni na
kufanya jumla ya shilingi 45milioni. Lakini barua hiyo haitaji kifungu cha
Kanuni Yanga au Ngasa aliyokiuka.
Yanga
inaiona adhabu hii kuwa ni ya uonevu, kwa Klabu na Mchezaji inayokiuka kanuni
za mashindano hayo, misingi ya sheria na haki za msingi za mlalamikiwa.
Mnamo tarehe
23/8/2013 Klabu ya Yanga Iliwasilisha rufaa yake TFF kupinga adhabu hiyo, na
sababu za rufaa hiyo ni kama ifuatavyo:-
1. KAMATI ILIKOSEA KIKANUNI NA KISHERIA
KUMWADHIBU NGASA KWA KUZINGATIA MKATABA BATILI
Suala la
usajili wa mchezaji Mrisho Ngasa baina yake na Simba Mara baada ya Msimu wa
2012/2013 kumalizika ulikuwa na matukio makubwa yaliyomhusu Mchezaji Mrisho
Ngasa, Klabu ya Simba na Klabu ya Azam. Kamati ya sheria na hadhi za wachezaji
ya TFF ilipaswa kuyarejea kabla ya kufikia uamuzi waliofikia hasa kwa
kuzingatia mchezaji hakuwepo kujitetea katika kikao hicho.
i. Tukio baada ya Mechi kati ya Yanga na
Azam Kumalizika katika msimu wa 2012/2013.
Baada ya
mechi hiyo hakuna asiyekumbuka mrisho Ngasa kuonesha mapenzi yake kwa Klabu ya
Yanga, baada ya kuvaa jezi ya yanga na kubebwa na mashabiki wa Yanga.
ii. Timu ya Azam Kutangaza kumpeleka Ngasa
Tukio la
Ngasa kuvaa Jezi ya Yanga halikuifurahisha Klabu ya Azam na kutoa mapendekezo
ya kumtoa kwa mkopo kwa klabu iliyokuwa tayari kutoa kiasi cha dola 50,000, na
yanga hawakuafiki kiwango hicho ndipo Simba walifanikiwa kumnyakua Ngasa kwa
Mkopo. Na klabu ya Azam iliutangazia umma wa wa Tanzania kumpeleka Ngasa kwa
mkopo katika klabu ya Simba.Kamati yako pia inaweza kufuatilia katika mtandao
wa Azam fc ( www.azamfc.co.tz).
iii. Tamko la Mrisho Ngasa Kushangazwa na
uamuzi huo pasipo kushirikishwa.
Baada ya
umma kutangaziwa uamuzi huo Mchezaji Ngasa alitoa tamko kwa umma kupitia vyombo
mbalimbali vya habari Tamko la Ngasa kutokuwa tayari kuuzwa kama mbuzi, kwani
hakushirikishwa. Klabu yake na Simba waliweka msimamo na Ngasa alitishwa kuwa
asingeenda Simba basi angekaa benchi mpaka mwisho wa Mkataba wake.
iv. Uamuzi wa Klabu ya Simba Kumkabidhi Ngasa
Gari na Pesa.
Baada ya
tamko hilo la Klabu ya Azam na Mchezaji Ngasa. Mchezaji huyo ina semekana
alitoweka na kufunga mawasiliano yake, lakini baadaye alionekana katika vyombo
vya habari vilivyoripoti tarehe 2/8/2012akiwa amepigwa picha akiandika mbele ya
Kiongozi wa Simba. Baada ya sinema hizo
Ngasa kwa unyonge alisikika akisema amekubali kucheza Simba. Na tarehe 3/8/2012
Ngasa aliripotiwa katika picha na Vyombo vya habari akiwa mbele ya gari
iliyosemekana alipewa na Simba.
v. Mkakati wa Azam Fc Kummuza Ngasa Katika
Klabu ya Elmerekh
Ikumbukwe
pia kuwa wakati akiwa katika mkataba wa mkopo baina ya simba na Azam, Simba
walifanya utaratibu wa kumumsajili Ngasa, usanii ni mnamo tarehe December 5,
2012 vyombo vya habari viliripoti Azam
yamuuza Ngasa kwa Elmereikh kwa $ 75,000 sawa na Milioni 120
Suala la
kujiuliza ni kwanini Mkataba waliotia Simba wa tarehe 2/8/2012, haukuizuia Azam
kumuuza Ngasa December 5, 2012? Jibu ni rahisi kwamba Mkataba haukuwa na nguvu
yeyote ya Kikanuni au kisheria kwa maana ya uhamisho na usajili wa wachezaji,
ndio maana Simba hawakupinga, lakini Ngasa alikataa na kujificha hata maafisa
wa timu hiyo walipofika Tanzania bila kuonana na Ngasa.
Katika
Mwongozo wa FIFA juu ya hadhi za wachezaji na masuala ya kinidhamu (FIFA
Manual; Players Status and Disciplinary Matters) kipengele cha 3(d) kinaeleza
wazi kuwa katika kuhakikisha uthibiti wa mkataba baina ya mchezaji na klabu,
mahusiano ya kiajira lazima yazingatie uwiano baina ya matakwa ya mchezaji na
ya klabu (yaani pande zote mbili).
Kifungu cha
3(f) cha Mwongozo huo unabainisha kuwa kuna vipindi viwili tu vya usajili,
katika msimu mmoja. Swala la kujiuliza Simba waliingia makubaliano na Ngasa
katika kipindi kipi mbali na kuwa katika mkopo kwa msimu mmoja?
Kimsingi
Mchezaji Ngasa hakuwa na mkataba halali na Simba inakuwaje Ngasa awajibishwe
kinidhamu na Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji kwa makubaliano ambayo
hayatambuliwi kikanuni na kisheria?
Hata kama
imebainika kuwa Mrisho Ngasa alikuwa na mkataba na klabu ya Simba, ni wazi kuwa
katika maelezo hapo juu hapakuwa na hiari ya mchezaji kuamua kuingia katika
mkataba.
Sheria ya
Mikataba ya Tanzaia Sura ya 345 kifungu cha 10 kinatanabaisha kwamba
makubaliano yote yanakuwa mkataba kama yamefanyika kwa hiari na uhuru wa kila upande. Kifungu cha 14 cha sharia hiyo
inaongeza kuwa makubaliano yanakuwa ya hiyari endapo yanafanyika pasipokuwa na
kulazimishwa au shuruti, pasipo kuwa na shinikizo, pasipokuwa na udanganyifu,
au makosa.
Kifungu cha
19 cha sheria ya mikataba inatanabaisha kuwa pale ambapo hiyari katika mkataba
inapatikana pakiwa na kulazimishwa au hiyari ,shinikizo, udanganyifu au makosa
basi mkataba huo unakuwa ni batilifu ( voidable) kwa upande ambao hiyari
ilipatikana kwa hila hizo hapo katika kifungu cha 19.
Je katika
suala hili endapo Ngasa alipewa fedha na gari kulikuwa na hiyari ya dhati?
Ikumbukwe kuwa Ngasa alitishiwa kuwa asipokubali kucheza Simba angekaa benchi
hadi mwisho wa mkataba wake.
Alikubali
kuingia mkataba akiwa katika upande dhaifu kimaamuzi/weak position, hata
mkataba kama ulikuwepo haukuwa na nguvu kikanuni na kisheria.
2. KAMATI ILIKOSEA KIKANUNI NA KISHERIA KUTOA
UAMUZI KWA USHAHIDI WA UPANDE MMOJA PASIPO KUMSIKILIZA MRISHO NGASA.
Ngasa
hakupewa nafasi ya kujitetea juu ya utata wa yanayosemekana makubaliano ya kumpa fedha, Ngasa anaelewa fika alikuwa kwa
mkopo Simba, na kwamba simba hawakuwa na uwezo kwa kanuni za usajili kumpa
mkataba wa usajili kwa wakati huo, suala hilo lingepata majibu mazuri kama
ngasa naye angepewa fursa ya kuelezea alivyouelewa mkataba huo.
Ngasa
hakuitwa, hivyo alinyimwa haki ya msingi ya kusikilizwa. Kamati ilithibitisha
vipi tuhuma za kupokea fedha na kufikia kutoa adhabu kali kama ile ya kurudisha
milioni 45 pasipo mtuhumiwa kusikilizwa?
Nakama
ilithibitisha Ngasa kupokea fedha ni kiasi gani? Na kama alipewa gari thamani
yake ni kiasi gani, hivyo vyote huthibitishwa kwa risiti au bank statement.
Hata Kanunu
za adhabu za FIFA katika kifungu cha kinasisitiza kabla ya kutoa adhabu lazima
mlalamikiwa apewe fursa ya kusikilizwa.
Haya mambo yote
yalipaswa kupatiwa majibu kabla ya kutoa uamuzi na adhabu kwa Yanga na Ngasa,
kwa kutopata maelezo ya Mchezaji, Kamati
imemnyima Ngasa haki ya msingi ya
kusikilizwa kabla ya Kuadhibiwa (Aud
auteram patem) -the right to be heard, wala hapakuwa na mtu wa kumtetea.
3. KAMATI ILIKOSEA KIKANUNI KUMWADHIBU
MCHEZAJI MRISHO NGASA KWA KUINGIA MKATABA NA SIMBA NJE YA KANUNI ZA USAJILI.
Hakuna shaka
Simba ilimrubuni mchezaji kwa kumshawishi asaini mkataba wa kuitumikia klabu
hiyo nje ya utaratibu wa usajili na bila woga waliuleta mkataba huo na kuweka
pingamizi.
Hata kanuni
za FIFA zimeweka adhabu kali kwa viongozi wanao gushi nyaraka za kuweka
mahusiano ya kisheria kama inavyodaiwa na Simba dhidi ya Ngasa, kwa kuwa
uhalali wa mkataba huo unatia mashaka kwa mujibu wa kanuni za usajili na adhabu
hutolewa kwa mujibu wa Chapter II,
Section 5 Article 61 ya Kanuni za Adhabu za Fifa (FIFA Disciplinary code) ina
tamka wazi kuwa endapo kutakuwa na udanganyifu au kugushi nyaraka zinazo
husiana na shughuli za mpira ikiwa aliyefanya hayo ni kiongozi adhabu yake ni
kufungiwa kwa uchache miezi 12.
Pia endapo
Klabu imekiuka taratibu za usajili kama zilivyowekwa kwa mujibu wa Kifungu cha
5 na 6 vya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa wachezaji za fifa na TFF.
Je endapo
alipewa fedha na gari je ilikuwa ni kwa ajili ya Usajili wa msimu huu au
kuridhia kucheza kwa mkopo akiwa mchezaji wa Azam.
Na kama
ilikuwa ni kwa ajili ya usajili wa Msimu huu kwa nini Azam FC tarehe 5/8/2012
waliamua kumuuza Ngasa Sudani na bila Simba kuleta malalamiko rasmi TFF?
Je mkataba
ulikuwa ni wa kuichezea Simba kwa msimu huu wa 2013/2014, mkataba huo
ulifanyika katika kipindi mahsusi cha kuingia mkataba na mchezaji au ni
makubaliano ya awali (MOU), kama ni makubaliano ya awali kamati hiyo haikupaswa
kujihusisha na makubaliano hayo. Kwa namna yeyote ile mkatabawa Simba na Ngasa
wa tarehe 2/8/2012 ulifanyika ndani ya mkataba wa mkopo na Azam na hivyo
mkataba wa Simba ukawa batili na ndivyo kamati ilivyoona.
Je, kamati
ilifanya sahihi kuutambua mkataba huo pasipo kumuuliza mchezaji na kuamuru
kurudisha fedha na fidia isiyo ya haki wakati kamati haitambui uhalali wa
mkataba huo?
Kama vile
kamati iliona haikuwa halali kuiadhibu Simba hivyo hivyo haikuwa na mamlaka
kikanuni kutoa adhabu kwa Ngasa kwa mujibu wa majukumu yaliyo ainishwa katika
Kipengele cha 40(8) cha Katiba ya TFF.
4. KAMATI ILIKOSEA KISHERIA KWA WALIOWEKA
PINGAMIZI KUWA SEHEMU YA KUTOA UAMUZI
Kamati
imekiuka haki ya msingi inayomzuia mtu kuwa jaji kwenye shauri lake
mwenyewe.(“Nemo Judex in causa sua”)
Kama
tulivyoeleza hapo awali, Simba ndio walioweka pingamizi na tuhuma za mkataba na
viongozi wa Simba walikaa katika kamati iliyoamua hatma ya Ngasa pasipo Ngasa
kuwakilishwa kwa vyovyote maamuzi hayangemtendea haki Ngasa.
5. KAMATI ILIKOSEA KIKANUNI KUINYIMA KLABU YA
YANGA KUMTUMIA NGASA KATIKA MECHI SITA PASIPO NA SABABU ZA MSINGI.
Kwa
kumfungia Ngasa mechi sita ni kuiadhibu Klabu ya Yanga kwa kosa ambalo kama
lipo haijahusika nalo, Klabu ya yanga imemsajili Ngasa kihalali hivyo kumfungia
Ngasa ni uonevu kwa Yanga.
Haikubaliki
kimantiki kutomruhusu Ngasa kuchezea Yanga wakati huo huo TFF wanamtumia katika
Timu ya taifa, kama ambavyo TFF/Timu ya Taifa haihusiki katika mkataba
batilifu, Yanga nayo haihusiki na makosa yeyote, hivyo ni uonevu kwa Yanga
kutomruhusu Ngasa kuitumikia katika mechi sita.
Ni rai yetu
nyenyekevu Kuomba kamati yako kuifutia Yanga adhabu ya kutomtumia mchezaji
Ngasa katika mechi tano zilizosalia, kwa kuwa katika suala hili Yanga anakuja
mbele ya kamati yako akiwa na mikono safi.
Imetolewa na:
Katibu Mkuu
Young
Africans SC.
0 COMMENTS:
Post a Comment