Na Saleh
Ally
Bingwa wa
dunia wa ngumi za kulipwa, Francis Cheka, anayetambuliwa na Shirikisho la Ngumi
la WBF, anasema hadi anafikia kubeba ubingwa huo kwa kumchapa Mmarekani, Phil
Williams, amepita mambo mengi ya kukumbukwa.
Williams ni
kinyozi lakini alikuwa fiti na kumpa Cheka wakati mgumu, ingawa baadaye
alifanikiwa kutwaa ubingwa huo akiwa Mtanzania wa kwanza kumchapa Mmarekani
katika ardhi ya Tanzania.
Cheka
anasema amekuwa akipitia mambo mengi katika mchezo huo na wakati mwingine
amekuwa akifikia hadi kukata tamaa akifikiria kuachana na mchezo huo, lakini
hawezi kufanya hivyo kwa kuwa ndiyo kazi yake.
“Mambo ni
mengi, huenda ni vigumu sana kwa mashabiki namna wanavyokwenda. Nimekuwa na
hofu kubwa wakati mwingine hadi kufikia kuwaza kwamba ninaweza kuacha mchezo wa
ngumi na kufanya mambo mengine.
“Mfano,
angalia katika pambano ambalo nilikwenda kucheza kule Ujerumani, nilikutana na
bondia mmoja anaitwa Uensal Arik ambaye naweza kusema si mbaya kwa maana ya
kuwa na uwezo.
“Lakini
baada ya kufika tu katika Mji wa Berlin, nikiongozana na wakala mmoja Mkenya,
nilianza kufanya mazoezi na kocha mmoja Mjerumani, nafikiri. Kama siku mbili
hivi, kumbe yule kocha akapeleka taarifa kwa yule mpinzani wangu kwamba mimi
nilikuwa mkali.
“Wakati
nikiendelea kusubiri pambano, yule bondia alituma watu na kuwataka wanishawishi
nichukue fedha halafu nimuachie anipige katika pambano hilo.
“Nilitaka
kujua ni kiasi gani, nikaelezwa ni euro 5,000 (nilipotaka kujua kwa fedha za
Tanzania, nikaambiwa inafika hadi Sh milioni 11. Niliona fedha nyingi sana na
huenda nikazihitaji sana kwa ajili ya maisha yangu.
“Lakini
nilisema nataka kutimiza ndoto zangu za kuwa bingwa na kushinda pambano langu
Ulaya, hivyo nikashikilia msimamo kwamba nilitaka mshindi apatikane pale
ulingoni bila ya hongo.
“Awali
nimewahi kusikia kuwa kuna mapromota wanawapeleka Watanzania wakashindwe na
kulipwa. Mimi sikukubaliana na hilo, halafu nilikuwa ninadai euro elfu tano za
pambano hilo. Hivyo nikajua nitazipata hizo na nilikuwa na uhakika wa kushinda.
“Sikupata
nafasi ya kuongozana na kocha wangu, walieleza kwamba nilitakiwa kwenda na
wakala ambaye ndiyo angekuwa msaidizi wangu ulingoni. Basi nilifanya hivyo
kweli na pambano lilianza na ukweli nilifanikiwa kutawala kuanzia raundi ya
kwanza hadi ya saba.
“Kilichonitokea
hadi leo sijawahi kusahau, yule msaidizi wangu ulingoni alirusha taulo ulingoni
eti nilikuwa nimezidiwa. Lakini haikuwa kweli, ukitaka nenda youtube uiangalie
ile video. Hali ile ilinitia shaka sana, niliona kulikuwa na njama yule Mkenya
alifanya.
“Huenda
yeye alifaidika na kushindwa kwangu, huenda baada ya kukataa walichoniambia,
labda walizungumza naye pembeni. Nilimueleza wazi kwamba alinimaliza, nilikasirika
na hata machozi yalinitoka,” anasema Cheka.
“Ajabu
zaidi, hadi leo sijapewa hata ile euro elfu tano kwa ajili ya kumalizia malipo
ya pambano hilo. Ajabu hata aliyenitafutia pambano amekuwa kimya na hanisaidii
lolote, kitu ninachoona si sahihi.”
Kingine
ambacho kinampa Cheka hofu katika maisha yake ya ngumi, anasema si ubabe wa
bondia yeyote anayekutana naye, badala yake ni kumaliza mchezo huo akiwa hana
hata fedha ya kuendeleza maisha yake.
“Bado
ninaona mabondia tunalipwa kidogo sana, kamwe siwezi kusema na kumlaumu Rashidi
Matumla. Kila siku amekuwa akilalamika, huenda watu wanaona kama alitumia fedha
vibaya, mimi naona tofauti kabisa.
“Mabondia
tunalipwa kiasi kidogo sana, fedha nyingi tunazolipwa zinaishia kwenye
maandalizi tu. Baada ya kucheza pambano unakuwa huna kitu tena na hii inatokana
na mabondia wengi kutokuwa na wadhamini wanaoweza kuwafanya wawe na fedha za
maandalizi na zile wanazolipwa zibaki kama sehemu ya kujiendeleza kimaisha.
“Najiangalia
naona kama nimebakiza miaka mitatu hivi ya kuendelea kucheza ngumi na kufanya
vizuri. Je, nina nini hasa kimaisha? Hapo ndiyo nimekuwa nikichanganyikiwa
sana, sitaki kufikia alipo Matumla sasa.
“Nataka
kumtumia Matumla kama somo, huyu jamaa mimi ninamheshimu sana tofauti na watu
wanavyofikiria, maana amenisaidia kuwa bora lakini nasikia uchungu ninapoona
hana maisha mazuri. Sitaki na mimi niwe hivyo na hata mabondia wengine
wanaofanya vizuri sasa wanapaswa kutafakari,” anasema Cheka.
Cheka,
maarufu kama SMG, anasema ataendelea kucheza ngumi za kulipwa, kwani pamoja na
mchezo huo kuwa ofisi lakini ana mapenzi makubwa sana, hivyo ataendelea
kujituma huku akihamasisha fedha nyingi zaidi kuwekezwa kwa wanaojituma kama
ilivyo kwake.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment