Kocha Mkuu
wa Simba Zdravok Logarusic, amemuulizia msaidizi wake Seleman Matola katika
mazoezi ya siku mbili akamkosa, lakini akamtumia ujumbe wa sifa anazotakiwa
kuja nazo katika timu hiyo.
Logarusic, ukipenda muite Loga, amesema mpaka jana
Jumanne asubuhi, ameshafanya mazoezi katika vipindi viwili tofauti bila
msaidizi wake huyo, lakini anataka atakaporipoti ajue anakuja kumsaidia kweli
ikiwemo kutoa ushauri, si kumsikiliza na kufuata kila kitu atakachosema.
Loga raia
wa Croatia, amesema atamfukuza mara moja msaidizi wake atakayekuwa na kazi ya
kusema “ndiyo mzee”, katika kila atakalomweleza, ambapo anataka atakapoona kuna
kitu hakiko sawa aweze kujenga hoja kwa kumshauri kwa lengo la kupunguza makosa
watakayoweza kuyafanya.
“Nimeanza
kazi rasmi jana (juzi) na leo (jana), pia nimekuja kazini, lakini katika siku
hizo mbili nimeuliza yuko wapi msaidizi wangu, nikajibiwa anakuja lakini
simuoni. Sitaki kuingia ndani sana katika hilo, lakini atakapokuja anatakiwa
kuelewa kuwa anakuja kunisaidia akiwa kama msaidizi wangu si kukubali kila
nitakachosema alisema Loga.
Matola
ambaye ni kocha wa timu ya vijana ya Simba, alipoulizwa jana sababu za kumfanya
achelewe kujiunga na timu kubwa, alisema:
“Bado niko
kwenye mazungumzo na uongozi kuhusiana na mkataba, tukimaliza vizuri basi
nitaanza kazi mara moja, hivyo kocha avute subira kidogo maana vizuri kuanza
kazi ukijua utaratibu.”
Taarifa
nyingine tulizozipata wakati tunaenda mitamboni zilieleza, Matola hakuwa na
mkataba Simba hata katika timu ya watoto anayoifundisha, hivyo alikuwa
anasubiri kusaini mkataba mpya kama kocha msaidizi.
0 COMMENTS:
Post a Comment