Wasanii watakaoshiriki tamasha la
Krismasi litakalofanyika Desemba 25, mwaka huu jijini Dar es Salaam, watamuenzi
rais wa kwanza wa Afrika Kusini, marehemu mzee Nelson Mandela kwa kusimama kwa
dakika moja kabla ya kuanza kutumbuiza.
Mwenyekiti wa kamati ya kuratibu tamasha
hilo, Alex Msama, alisema jana kuwa wasanii hao watafanya tukio hilo kutokana
na ukweli kwamba Mandela alitoa mchango mkubwa katika kuleta amani ya dunia na
hivi leo ulimwengu unashuhudia Afrika Kusini isiyo na machafuko.
“Mandela ni alama ya amani, waimbaji wa
Injili wanahusika sana katika kuhubiri amani ya dunia miongoni mwa mataifa. Kwa
kutambua ukweli huu, wasanii hao watasimama kimya kwa dakika moja kumuenzi
shujaa huyu pamoja na watu wote watakaohudhuria tamasha hilo,” alisema Msama.
Tamasha hilo litakalofanyika katika
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam litawakutanisha wasanii kama Rose Muhando,
Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, John Lisu na New Life Band kutoka Tanzania
wakati wasanii wa nje ni pamoja na Solly Mahlangu, Liliane Kabaganza, Solomon
Mukubwa na Ephraim Sekeleti.
Mzee Mandela alifariki dunia Alhamisi
iliyopita akiwa na umri wa miaka 95 nyumbani kwake jijini Johannesburg baada ya
kusumbuliwa na maradhi ya mapafu kwa muda mrefu. Anatarajiwa kuzikwa Jumapili
hii kijijini kwake Qunu.








0 COMMENTS:
Post a Comment