Na Saleh Ally
MALUMBANO ya Coastal Union umeyasikia, uongozi umekuwa ukielezea
kila kinachoendelea kuhusiana na mambo ndani ya klabu hiyo maarufu katika Jiji
la Tanga na nchini kote.
Hakuna anayeweza kukataa kuhusiana na umaarufu wa Coastal, lakini
hakuna mwenye akili timamu anaweza akawa anafurahia mwenendo wa kikosi cha timu
hiyo katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-14 hasa kama ana mapenzi nayo. Sasa
kero ndani yake ni malumbano.
Malumbano yaliyotawala ni kati ya uongozi na mfadhili wao, Nassor
Bin Slum ambaye anajulikana kama Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal Union ingawa
hivi karibuni Mwenyekiti wa Coastal, Ahmed Aurora alisisitiza kwenye vyombo vya
habari kwamba cheo hicho alijibandika!
Achana na cheo hicho ambacho inaelezwa kuwa Bin Slum alijibandika,
Aurora ameeleza kwamba Bin Slum kupitia makampuni yake amekuwa akijitangaza tu
bila hata ya kuingia mkataba na klabu hiyo, maana yake anajifaidisha tu!
Lakini wakati malumbano hayo yanaendelea, usisahau kuna mengine,
kuna baadhi ya vijana mashabiki wa Coastal wanataka kupewa kadi za uanachama,
lakini jambo lao linaonekana kuwa gumu kwa kuwa Katibu Mkuu, Kassim El Siagi
amekuwa haonekani ofisini lakini ajabu zaidi, uongozi wa Coastal Union
umepitisha jambo ambalo halipo kwenye katiba.
Kwamba anayetaka uanachama lazima ajadiliwe kwanza kabla ya
kupewa, lakini cha kushangaza zaidi fomu tu za kuchukua uanachama zinauzwa
shilingi 10,000 kitu ambacho ni kichekesho cha karne!
Yanga na Simba, ada ya mwanachama kwa mwaka ni Sh 12,000. Halafu
Coastal Union ambayo inayopaswa kuwa na mbinu kuwashawishi wanachama kwa wingi
kuingia ndiyo inafanya mambo yanayozuia wanachama kuingia.
Taarifa zinaeleza kuwa hofu ya viongozi wa Coastal wanahofia
vijana kuingia kwenye uanachama kwa kuwa watagombea katika nafasi zao na
kuwang’oa. Kama ni hivyo huo ni upuuzi wa karne na hatupaswi kuwa na viongozi
wa mwendo huo kwa kipindi hiki.
Ukifuatilia kwa karibu, malumbano yote yanayoendelea ni ya
kipuuzi, yanavyokwenda utafikiri hayajumuishi watu wazima ambao wanapaswa
kufikiria kwamba walipoifikisha klabu na kikosi chao, ni mbali na wanachotakiwa
ni kuendelea kuungana na kuendeleza na si kuendekeza malumbano.
Ukirudi kwenye malalamiko ya uongozi kuhusiana na Bin Slum,
unaweza kumuita mwanachama huyo wa Coastal ni mpuuzi.
Maana uongozi unasema Bin Slum amezitangaza kampuni zake kupitia
Coastal Union bila ya mkataba na hakuwa akitoa chochote, hata kwa kuangalia
inasikitisha!
Hakuna asiyejua kuwa Bin Slum ndiye amekuwa akifanya usajili wa
wachezaji wa timu hiyo, hata kama viongozi wa Coastal, leo, wanajaribu
kukanusha kama ambavyo walivyosema kuwa alijivika cheo cha mkurugenzi wa ufundi.
Baadaye akajitokeza kiongozi mwingine na kusema walimpatia wao na
siku waliyomkabidhi aliyeomba dua ya kuitakia timu yao mema alikuwa mwenyekiti
wa klabu!
Achana na usajili, zungumzia kambi ya kisasa ya Coastal ambayo
wachezaji walikuwa wakiishi mjini Tanga. Hata Simba hawakuwa na kambi kama hiyo
lakini leo inaonekana alijitangaza bure.
Rudi kwenye safari ya Oman, nakumbuka Simba ilitumia zaidi ya Sh
milioni 60 katika kambi ya Oman. Coastal Union walikaa siku chache, angalau
itakuwa Sh milioni 30 au zaidi, lakini bado unaweza kusema amejitangaza bure!
Kinachoibuka kutoka ndani ya Coastal kwa sasa ni majibu ya
kilichotokea hadi timu hiyo pamoja na usajili bora lakini bado ikaishia kushika
nafasi za chini kuliko wengi walivyotarajia. Je, tumuite au tuonyeshe jamii Bin
Slum ni mpuuzi kutokana na alichokifanya kwa klabu hiyo kongwe? Si sahihi,
kuweni waungwana, kuweni na mioyo yenye tabia ya kukubali ukweli na uzuri wa
waliofanya mazuri.
Mmoja wa wanachama wa Coastal amesema jeuri ya uongozi na dharau
kwa Bin Slum imetokana na uongozi kuanza kupata Sh milioni 100 za udhamini wa
Azam FC na zile za Vodacom. Hivyo wanaona wanaweza kujiendesha, hawamhitaji na
akiwa mbali, hawezi kuhoji wametumia vipi hizo za udhamini, hivyo wana nafasi
ya kufanya wanalotaka.
Mwenyewe Bin Slum kwa msimu mmoja, amesema ametumia Sh milioni 300
kwa ajili ya Coastal. Ndiyo maana nauliza, huyu Bin Slum ni mpuuzi, vipi
akapokee matusi na kebehi wakati angeweza kutoa nusu ya fedha hizo akaweza
kupata timu ya kuidhamini kama Mbeya City au hata Yanga na Simba, hata wakisema
wanaweka jina la bidhaa yake mgongoni.
Baada ya kutafakari nikagundua upuuzi alionao Bin Slum ni mapenzi
ya dhati! Anaipenda Coastal kwa kuwa ni klabu ambayo amekuwa akiipenda tokea
akiwa ‘kula kulala’ hadi sasa akiwa ni mtu anayejitegemea, anayejiweza na
anaweza kusaidia wengine.
Mapenzi hayo ya dhati ndiyo yanamfanya aangukie kwenye dharau kutoka
kwa watu ambao wana nia ya kujisaidia kuliko kusaidia. Najua wako ambao wana
hofu na viongozi wa Coastal ambao huenda wakalaumu au kuanza kusema fulani
amewakosoa kwa kuwa anatumiwa na Bin Slum, mimi sihofii hata kidogo kwa kuwa
nembo yangu ni kusema kweli tu, bila ya kona.
Katika maendeleo ya soka ya Tanzania, tunawahitaji watu kama kina
Bin Slum, watu wenye mapenzi, walio tayari kusaidia na waonyeshwe upendo. Sikubali
Bin Slum akitoa fedha, basi awe ndiyo mwenye kauli ya mwisho kwenye timu, yeye
si kiongozi wa kuchaguliwa, lakini vizuri kusikiliza mawazo yake.
Kwa Sh milioni 300 au hata nusu yake, Bin Slum alikuwa na haki ya
kutangaza kampuni yake na Coastal wanapaswa kuonyesha heshima kwake kwa kuwa
Mwenyekiti Aurora au Katibu wake, El Siagi walipaswa kutanguliza hadharani neno
ahsante kuliko kashfa na maneno yasiyo na tija ambayo wanazungumza kwenye
vyombo vya habari.
Ukiuliza kosa la Bin Slum, utaambiwa kampuni yake imejitangaza
bure, lakini hakuna anayekataa kuwa alikuwa akitoa fedha zake, sasa hiyo ni
bure vipi!
Lakini kama alijitangaza bure, basi inaonyesha kiasi gani viongozi
hao walikuwa wazembe na wanatakiwa kutumia vizuri busara na kuacha kutangaza
madudu waliyoyafanya, kama mtu alitangaza bure basi ni uzembe wao, si wa
mtangazaji!
Bado angeweza kutumia robo ya fedha hizo na kutangaza kwenye
mabango makubwa au kwenye vyombo vya habari na bidhaa zake zikatangazika. Msimuone
mpuuzi, mkubali alichofanya hata kama kidogo lakini ni bora.
Mkianza kumkimbiza yeye, nani tena atakuwa tayari kujitolea wakati
anaona fadhila inakuwa ni dharau na kashfa. Hata kama ni mpuuzi kutokana na
kusaidia kwake, basi malipo ya matangazo hayo angalau yanaweza kumpoza.
Ukiniambia nimpe ushauri Bin Slum katika hili, ninaweza kumuambia
maneno haya, mwisho uamuzi utakuwa ni wake: “Coastal Union ni timu yako kama
ilivyo kwa Aurora na El Siagi, kamwe usithubutu kuiacha kwa kuwa ni sawa na
mume anayejaribu kumsusa mkewe, akisikia anazidi kupata mateso ndiyo anamrudia,
hajui kabla hajamrudia alipotelea wapi na amepita wapi.
“Wazo zuri ni kuamini wewe ni mhusika, pole kwa maumivu ya dharau,
lakini si Coastal wote wanakudharau, naamini wengi wanatambua vitu bora ulivyofanya.
Lakini umepata funzo kwa kuwa kama ni udhamini, sasa uwe wa maandishi na
ikishindikana unaweza kuidhamini timu nyingine uendelee kusaidia soka ya
Tanzania inayosuasua na iliyojaza watu kibao wanaotaka kujiendeleza wao.
“Watu kama wewe bado wanahitajika sana na kwa Coastal, kama ni misaada
yako ya kawaida kama mwanachama si lazima iwe fedha, iendelee ili kuinusuru kwa
kuwa mchango wako umeonekana hasa kwa wale wakweli, waungwana na wenye tabia ya
kusema ahsante.”
Ushauri wangu wa mwisho kwa Coastal kama klabu na hasa viongozi,
wanapaswa kuonyesha ukomavu na utambuzi wa wanachokiongoza, kihistoria, klabu
hiyo ni kubwa.
Hivyo, hawapaswi kuwa watu wanaozungumza maneno tu ilimradi,
wanaoendeleza malumbano lukuki na mwisho ni kuidhalilisha klabu hiyo kongwe
ambayo inahitaji viongozi wenye busara ya juu wanaoweza kufanya mambo yaende
vizuri.
Nyie na Bil Slum, bado mngeweza kujadili masuala yenu kimyakimya,
ingawa kwa upande mwingine niwashukuru kwa ‘kuropoka’ kwenu, maana mmesaidia
watu kujua madudu yenu.
Kwa mwendo wenu, Coastal itarudi kulekule ilipokwama kwa zaidi ya
miaka nane. Pia kwa wanachama ambao wana maneno mengi sana kuliko vitendo,
wanaolaumu fulani kaitumia klabu au vile wakati hawachangii lolote, hawana hata
wazo moja, nao wajirekebishe, vitendo ndiyo husababisha mabadiliko na si maneno
huku mkiwa mmekaa kwenye vijiwe vya kahawa.
0 COMMENTS:
Post a Comment