Kampuni ya Azam Media
imetangaza kuwa tayari imeshatuma fedha kwa Bodi ya Ligi kwa ajili ya msimu wa
ligi wa Vodacom kwa mwaka 2014/ 2015.
Fedha hizo zimetolewa mapema zaidi
kwa ajili ya kusaidia maandalizi mapema kwa timu kama ilivyokubaliwa kwenye
mkataba wa miaka mitatu ya udhamini wao katika ligi hiyo.
WAKIPONGEZANA |
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Azam zilizopo Tazara, Dar es salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Rhys Torrington, alisema kuwa kampuni hiyo inavutiwa na aina nzuri ya ushirikiano kati yake na bodi ya Ligi.
Alisema kuwa kupitia bodi hiyo Azam imepiga hatua kubwa katika kufanikisha adhma yake ya kuifanya Ligi hiyo ya Vodacom kuwa ya kuvutia zaidi.
“Ligi hii tunataka kuifanya kuwa ni
moja kati ya ligi zinazovutia na kuonesha ushindani barani Afrika, ingawaje
ninajua kuwa kuna mengi ambayo yanatakiwa kuendelea kufanywa ili kuipa nguvu
zaidi ligi hii”alisema Torrington.
Alisema kuwa kwa kutambua hilo ndio
maana Azam Media imehakikisha kuwa klabu zote zinapata fedha mapema ili
kusaidia suala zima la maandalizi.
Akizungumzia mikakati ya baadae ya
Azam Media alisema kuwa inatarajia kuanza kuonesha soka la mitaani (street
soccer) mbalimbali moja kwa moja (live) itakayokuwa ikiendelea kwenye nchi za
Kenya na Uganda.
Alisema kuwa kwa sasa Azam Media
imeanza kujikita katika nchi za Kenya, Uganda na Malawi ambapo itakuwa ikiuza
ving’amuzi vyake katika nchi hizo.
Aliongeza kuwa pia katika kuhakikisha
kuwa inatoa mwanya zaidi wa vipindi vizuri na vya kuvutia inaendelea na vipindi
vya michezo vya Morning Trumpet, sport@8 pamoja na Kwetu House.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu
wa Bodi ya ligi, Silas Mwakibinga alisema kuwa kwa hatua hiyo ya Azam ya
kuhakikisha upatikanaji wa fedha hizo kwa wakati ni nzuri na itasaidia
kuzipatia timu muda mzuri wa kujiandaa.
Alisema kuwa bodi yake inavutiwa sio
tu na utangazaji wa vipindi unaofanywa na Azam bali pia hata nia yao ya
kuendeleza soka la Tanzania.
Azam Media ilisaini mkataba wa miaka mitatu na wenye
thamani ya TSHS 5,560,800,000 kuonesha mechi za live na za kurekodi mechi za
Ligi Kuu na fedha hizo zinalipwa kwa awamu tatu.
0 COMMENTS:
Post a Comment