Mshambuliaji wa zamani nyota wa Sigara, Gebo Peter
atazikwa
kesho mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa marehebu, Spear Mbwembwe,
mwili wa marehebu utasafirishwa kesho alfajiri kwenda Morogoro.
Gebo amefariki baada ya kufanyiwa upasuaji wa henia katika
hospitali ya Mwananyamala siku chache zilizopita.
Lakini baadaye akahamishiwa Muhimbili ambako kuanzia juzi hali
yake ilizidi kuwa mbaya hadi alipohamishiwa Chumba cha Watu Mahututi (ICU) na
leo alfajiri mauti yakamkuta.
TFF yatoa
rambirambi…
RAMBIRAMBI MSIBA WA GEBO PETER
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Simba na
Taifa Stars, Gebo Peter kilichotokea usiku wa kuamkia leo (Juni 6 mwaka huu)
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
Gebo aliyezaliwa mwaka 1961, pia aliwahi
kuchezea timu za Sigara ya Dar es Salaam, CDA ya Dodoma na kombaini ya Mkoa wa
Dar es Salaam (Mzizima United). Hadi mauti yanamkuta alikuwa akijishughulisha
na biashara, kubwa ikiwa ya vifaa vya michezo.
Msiba huo ni mkubwa katika familia ya
mpira wa miguu nchini kwani, Gebo enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa
mchezaji na baadaye kiongozi katika timu ya Manyema ya jijini Dar es Salaam.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu
Gebo Peter, klabu ya Manyema na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam
(DRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha
msiba huo mzito.
Msiba upo nyumbani kwao Vingunguti
karibu na Kanisa Katoliki ambapo taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na
familia.
Marehemu ambaye ameacha mjane na watoto
watatu anatarajiwa kuzikwa kesho (Juni 7 mwaka huu) nyumbani kwao Kigurunyembe,
mjini Morogoro.
Bwana
alitoa, na Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Amina
0 COMMENTS:
Post a Comment