Mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, kutoka
nchini Brazil, Andrey Coutinho, jana aliwapiga darasa washambuliaji wa timu
hiyo, Jerry Tegete na Hussen Javu, akiwaonyesha jinsi wanavyotakiwa kupokea
mpira wanapokuwa ndani ya eneo la hatari.
Coutinho ambaye sasa ana wiki mbili tangu ajiunge
na Yanga, alifikia hatua hiyo, baada ya washambuliaji hao mara kwa mara
kushindwa kumalizia kwa ustadi mkubwa mipira ya krosi ambayo alikuwa
akiwapigia, wakati wa mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari
Loyola, Mabibo jijini Dar es Salaam.
Kutokana na hali hiyo, Coutinho alilazimika
kuwaonyesha wachezaji hao jinsi ya kuzitumia nafasi hizo kwa kutumia kichwa
kuunganisha krosi hizo alizokuwa akiwapigia, lakini pia pale wanapoona hawawezi
watumie kifua kumiliki mpira.
Hata hivyo, Tegete na Javu walionekana kumuelewa
mchezaji huyo na kuufanyia kazi ushauri wake na baada ya muda, wakafanikiwa
kuzifumania nyavu.
Hata hivyo, baada ya hali hiyo, kocha mkuu wa
timu hiyo, Mbrazili Marcio Maximo, alilazimia kuwakusanya wachezaji wote na
kuwapa mazoezi ya kufunga wakiwa nje ya eneo la hatari kwa kugongeana pasi
mbili kisha kupiga shuti langoni.
SOURCE: CHAMPIONI








0 COMMENTS:
Post a Comment