Kiwango cha juu anachoonyesha mazoezini kipa wa
Yanga, Juma Kaseja, kimemvutia zaidi kocha mkuu wa timu hiyo, Mbrazili, Marcio
Maximo, hali ambayo inamweka kwenye wakati mgumu aliyekuwa kipa chaguo la
kwanza, Deogratius Munishi ‘Dida’, ambaye sasa yupo na timu ya taifa, Taifa
Stars.
Hali hiyo imemfanya Kaseja ambaye yupo na
kikosi cha Yanga kinachoendelea na mazoezi yake ya kujiandaa na msimu ujao wa
ligi kuu, kuzidi kujifua mbele ya Maximo ili aweze kujitengenezea mazingira
mazuri yatakayomfanya awe kipa chaguo la kwanza.
Kocha wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali,
ameliambia gazeti hili kuwa, Dida atakaporudi katika kikosi hicho, atakuwa na
kazi kubwa ya kufanya ili aweze kumshawishi Maximo kama ilivyo sasa kwa Kaseja
ambaye anaonyesha kiwango kizuri mazoezini.
“Binafsi nawaamini makipa wote watatu wa
kikosi chetu ambao ni Kaseja, Dida na Barthez (Ally Mustapha), wana uwezo wa
juu.
“Lakini ili waweze kupata nafasi katika kikosi
cha Maximo, inabidi wapambane na hivi sasa Kaseja anaendelea vizuri, hivyo Dida
atakaporejea kutoka timu ya taifa, anatakiwa kuonyesha kuwa anaweza.
“Kama akisinzia basi wenzake wanaweza kumshusha
kwa sababu wanafanya vizuri hivi sasa mazoezini,” alisema Pondamali.








0 COMMENTS:
Post a Comment