Na Saleh Ally
KUNA mzozo mkubwa ikiwa ni siku chache tu baada ya
kwisha kwa michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika nchini Brazil na Wajerumani
kuibuka na ubingwa kwa kuifunga Argentina kwa bao 1-0 katika muda wa nyongeza.
Ujerumani walistahili, hakuna hata mmoja anayeweza
kulalama. Tofauti na tuzo ya mchezaji bora ambaye ameitwaa Lionel Messi, wengi
wanapinga hasa kutoka barani Ulaya.
Waingereza ambao timu yao iling’olewa hatua ya
makundi, ndiyo wamelivalia njuga, kizuri zaidi hawasemi alistahili kuibeba
Wayne Rooney lakini wanasisitiza kwamba angalau Toni Kroos, kiungo maestro wa
Ujerumani au kinda James Rodriguez angeweza kuchukua tuzo hiyo.
Wanaweza kuwa na hoja, lakini lilionekana ni jambo la
kupita, badala yake wamelifanya hoja hadi kufikia baadhi ya wachezaji wa
Amerika Kusini wakiwemo nyota wa Argentina, nao wamekuwa wakipewa maswali
yatakayotimiza wanachotaka Wazungu hao.
Wako wanaosema Arjen Robben wa Uholanzi au Thomas
Muller wa Ujerumani ndiyo waliostahili. Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa)
limejaribu kutoa ufafanuzi lakini ukweli Messi alistahili.
Angalia hii:
Kuanzia mwanzo wa michuano, Messi alionyesha ni
nahodha wa ushindi, kiwango cha Argentina hakikuwa kati ya vilivyopewa nafasi
ya kuchukua kombe, lakini Messi ndiye alionekana ni uhai.
Akitokea katika hali ya kusuasua kutokana na majeraha
yaliyomfanya kutofanya vizuri katika kikosi cha Barcelona msimu uliopita, Messi
ndiye alikuwa chagizo la kuipeleka Argentina kwenye fainali Maracana.
Alifunga na kutoa pasi wakati wa ushindi wa mabao 2-1
dhidi ya Bosnia and Herzegovina. Mechi dhidi ya Iran wakabana vilivyo, lakini
uwezo binafsi akafunga bao pekee na wakapata pointi tatu muhimu, wakavuka hadi
16 bora.
Hatua ya 16 ilikuwa dhidi ya Nigeria, kama unakumbuka,
walikuwa 2-2 na mechi ilikuwa ngumu lakini haikuishia hapo, angalia uwezo
binafsi wa Messi kukimbia na mpira kwa kasi ya juu na kutoa pasi ya bao kwa
Angel Di Maria katika dakika ya 118 iliyozaa ushindi dhidi ya Uswisi na
Argentina ikatinga nusu fainali kwa ushindi wa bao 1-0.
Nusu fainali haikuwa lelemama dhidi ya Uholanzi
waliokuwa wamekamilika vilivyo, dakika za nyongeza pia hazikusaidia, hivyo
wakasonga kwenye mikwaju ya penalti. Usisahau pamoja na kuwapa wakati mgumu
mabeki wa Waholanzi hao, Messi alifunga moja ya penalti muhimu zilizoipeleka
Argentina fainali wakati wengi waliamini siku hiyo ingelala hata kwa mabao
sita.
Fainali pia mambo hayakuwa na tofauti, Ujerumani
ilikuwa imeibutua Brazil kwa mabao 7-1. Fainali ilikwenda muda wa nyongeza hadi
Mario Gotze alipofunga bao katika dakika ya 113.
Utaona kila mechi Messi alishiriki kikamilifu, hata kama
ana mabao manne ya kufunga na anazidiwa mawili na Rodriguez, haikuwa rahisi
kumuangusha kutwaa tuzo hiyo.
Muller alikuwa kwenye kikosi cha Ujerumani ambacho
hata asingekuwepo nani, kilikuwa bora bado, Messi alikuwa mmoja anayebeba
kikosi kizima.
Kwa hali halisi, alistahili hiyo tuzo lakini Wazungu
watakuwa wanachukizwa na hilo kwa kuwa alitaka achukue mchezaji kutoka Ulaya na
hata ile hali ya kumtetea Rodriguez ni sehemu tu ya kutaka kupatikana kwa
msisitizo kwamba Messi hakustahili!
Baada ya Messi aliyeshika nafasi ya pili ni Muller na
Robben akachukua ya tatu na utaona, Muller anapewa kwa kuwa timu yake imefika
fainali sawa na Messi unapomlinganisha na Rodriguez. Wazungu bana!
KIATU CHA DHAHABU:
James Rodriguez (Colombia)
Bao 6, pasi 2 za mabao
KIATU CHA SILVA:
Thomas Muller (Ujerumani)
Bao 5, pasi 3 za mabao
KIATU CHA SHABA
Neymar
Bao 4, pasi 1 ya bao
GLOVU ZA DHAHABU
Manuel Neuer (Ujerumani)
MCHEZAJI BORA KINDA:
Paul Pogba (Ufaransa)
TUZO YA FIFA YA FAIR PLAY:
Colombia








0 COMMENTS:
Post a Comment