July 18, 2014




Na Saleh Ally
BURUDANI ya Kombe la Dunia hata kama ni utamu, basi ndiyo ule unatoweka mdomoni kama mtu aliyeanza kutafuna Big G, baada ya muda, kutafuna kunabaki fasheni tu, utamu unakuwa umepotea.


Uzuri ni kitu kimoja, kila baada ya utamu huu, unafuatia ule. Baada ya Kombe la Dunia, sasa macho, masikio yanaelekezwa upande mwingine, ligi za nchi mbalimbali.

Unapoangalia ligi za nchini mbalimbali ni vigumu sana kuanzia kwingine, hauwezi kukwepa Ligi Kuu England maarufu kama Premiership.

Ina mengi ya kujifunza ambayo kwa wale wanaoshiriki Ligi Kuu Bara, mfano Bodi ya Ligi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), viongozi wa klabu, makocha, wachezaji na hata mashabiki wanaweza kujifunza.

Msimu uliopita watu milioni 13.9, unaweza kusema milioni 14 walishuhudia mechi 380 za Premiership. Wastani wake ni watu  36,657 kwa mechi moja. Hapa tu unaweza kujifunza kuwa kwa ligi yetu nyumbani wameingia watu wangapi.

Idadi ya watu milioni 14, maana yake ni zaidi ya raia wote wa Rwanda, ndiyo waliingia viwanjani kushuhudia mechi za ligi hiyo. Nakuhakikishia, asilimia 2 au 3 watakuwa ni Watanzania wanaosafiri hadi Uingereza kushuhudia mechi za ligi hiyo.

Hawafuati kingine, badala yake ni burudani inayoridhisha mioyo yao, ndiyo maana utajiri mkubwa unazidi kuongezeka katika ligi hiyo, kwa kuwa watu kibao kutoka mataifa katika Bara la Afrika, Asia na kwingineko wamekuwa wakitoa fedha zao kwenda England.

Lazima kuwe na hamu ya mafanikio hata kwa kiwango cha chini lakini watu kuingia kwa wingi uwanjani, lazima kuwe na viwanja bora, sehemu ya kukaa na kuchezea. Timu pia zionyeshe soka safi litakalowavuta wengi.

Haya yanawezekana kama kukiwa hakuna migogoro, watu wenye tamaa za kushibisha matumbo yao badala ya mafanikio ya soka lenyewe na ikiwezekana makomandoo wote ‘wafe’ ili soka lipande kwa kuwa England hakuna hata mmoja soka linaendelea.

Maneno mengi ya nini! Taratibu kwa wakati wako soma takwimu za Premiership msimu uliopita, uone utamu wake na huenda msimu ujao zikapanda. Je, hapa nyumbani tunazo takwimu za kutuonyesha na tunajua kuwa tunapanda au tunateremka? Hodi England.

MSIMU WA 2013–14

Mabingwa: Man City
Mechi zilizochezwa: 380
Mabao yaliyofungwa:            1052 (mabao 2.77 kwa mechi)
Mfungaji Bora: Luis Suarez (mabao 31)

Kipa Bora: Petr Čech & Wojciech Szczęsny (wote mechi 16 bila kufungwa)

Ushindi mkubwa nyumbani: Man City 7–0 Norwich
Ushindi mkubwa ugenini: Tottenham 0–5 Liverpool
Mechi zenye mabao mengi: Man City 6–3 Arsenal
                                            Cardiff City 3–6 Liverpool

Ushindi mfululizo: Liverpool (Liverpool-mechi 11)
Mechi nyingi bila kufungwa: (Liverpool-mechi 16)
Mechi nyingi bila kushinda: (Fulham&Sunderland, Wes Brom-mechi 9)
Vipigo vingi mfululizo: (Crystal Palace-Mechi 7)
Watu wengi uwanjani: 75,368 (ManU 4–1 Aston Villa)
Watu wachache uwanjani: 19,242 (Swansea 3–3 Stoke)
Jumla ya walioona Premiership viwanjani: 13,929,810
Wastani kwa mechi: 36,657


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic