July 18, 2014




MESUT Ozil wa Arsenal aliamua kutoa fedha zake alizopata kwa kama ‘bonus’ kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwa watoto wenye matatizo wa Brazil.
Pauni 240,000 (Sh milioni 600) alizopata kutokana na Ujerumani kushinda Kombe la Dunia kwa kuichapa Argentina kwa bao 1-0, akaziacha Brazil. Awali ilielezwa kuwa alifanya hivyo kwa watu wa Gazza, mwakilishi wake akafafanua.


Huenda wengi waliamini alifanya hivyo kwa kuwa yeye ni Mwislamu, lakini ukweli alizitoa fedha hizo Brazil ambako ni nchi ya Wakristo wengi.

Siku moja baada ya Ozil kufanya hivyo, kiungo mkongwe Javier Mascherano akawashauri wenzake wa Argentina walioshika nafasi ya pili kutoa kiasi chao cha fedha, wakakubali, wakatoa.

Argentina walitoa pauni 80,000 (Sh milioni 200) kwa Hospitali ya Kansa ya Garrahan ya kwao Argentina. Mambo haya mawili ni ya kujivunia kabisa katika mchezo wa soka.

Mimi kama mpenda soka, mdau wa soka na mtu ninayepambana kwa ajili ya mchezo huo kwa moyo wa kuona mafanikio nasikia raha, pia ninasikia wivu tena wa kiwango cha juu sana.

Najiuliza bila ya kuwa na jibu, kuwa wachezaji wa Tanzania au klabu zao zinazoshiriki Ligi Kuu Bara au Ligi Daraja la Kwanza, wamewahi kufikiria suala la kusaidia jamii?

Jamii ndiyo kila kitu, matatizo ya watu yanawahusu na wao kama nyota au ambao angalau wamejaaliwa nafasi kidogo na mwenyezi Mungu amewanyoonyesha neema, wanawaza kuokoa wengine.

Wachezaji wa Tanzania hawapati kikubwa kama cha Ozil au Argentina kwa kuwa bado wako kwenye viwango vya chini na hata soka yetu ni ya ridhaa.

Lakini kusaidia hakujali idadi au wingi, msaada ni msaada tu na hasa ukitolewa kwa nia ya dhati, kwa kulenga kusaidia, basi ni msaada na unapaswa kupolewa au kuheshimiwa.

Imani za dini zinasisitiza kutoa bila ya kusema au kutangaza, mimi sipingi lakini ninaona ni bora wakati mwingine watu wakajua ili kuhamasika kuiga au kufuata kilichofanywa.

Kilichofanywa na mitume, leo tunatakiwa kuchukua kama mifano, tuko tayari kufuata kwa kuwa tumepewa na kuelezwa sifa zao.

Wachezaji si mitume, lakini ni watu wanaoheshimiwa, wenye watu wanaowakubali na kuwaunga mkono, hivyo wakisaidia itakuwa rahisi sana kuwashawishi wengine kufanya mambo hasa yale ambayo ni mema.

Wachezaji wa Tanzania na hata viongozi wao wanaweza kushawishika na hili, wakaingia kusaidia jamii yao hata kwa kidogo walichonacho.

Fedha inaendesha hii dunia, lakini ukiifikiria huwa ni kitu cha kuja na kwenda, lakini ubinadamu hubaki kwa mwanadamu hadi siku ya mwisho ya maisha yake.

Mungu anapokuongezea au kukujaalia kupata ahueni kwenye maisha, hawezi kukuagiza kwa nguvu usaidie. Jipime na utafakari kama kweli wengine wanaweza kufa njaa au kuandamwa na shida bila ya msaada.

Wagonjwa wa kansa kama walivyofanya Argentina au watoto wenye matatizo kama alivyoamua kusaidia Ozil, wote wanahitaji msaada na wapo kwa wingi hapa nyumbani kwetu Tanzania.
Wale wa Argentina wamesaidiwa na Waargentina, Wale wa Brazil wamesaidiwa na Ozil. Si vizuri kusubiri Ozil mwingine aje Tanzania kuwasaidia Watanzania.
Staa wa Tanzania wana uwezo wa kuwasaidia Watanzania na hili linawezekana bila ya shida yoyote, tafadhali fanyeni kwa ajili ya nchi yetu ambayo wakati mwingine haihitaji msaada na inaweza kujisaidia.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic