July 7, 2014



BAADA ya taarifa kuwa Neymar wa Brazil hatacheza mechi mbili za Kombe la Dunia zilizobaki, hisia tofauti za mashabiki zilitawala na sherehe za Brazil kufuzu hatua ya nusu fainali, hazikuwa gumzo kubwa.


Beki wa Colombia, Juan Camilo Zuniga ,28, akachukua nafasi, mashabiki wa soka katika vijiwe mbalimbali na mitandano ya jamii wamekuwa wakitofautiana kuhusiana na faulo aliyoifanya Zuniga dhidi ya Neymar na kumvunja mfupa mdogo wa uti wa mgongo.

Mashabiki wengi wa Tanzania, wanaamini Zuniga ambaye anakipiga Napoli ya Italia si mtu mzuri kwa kuwa amewanyima burudani ya kumuona Neymar ,22, katika mechi mbili zilizobaki, yaani nusu fainali na fainali au mshindi wa tatu.

Lakini kwa wale wa Brazil, hisia ni zaidi ya kawaida, Zuniga ni adui wa taifa, Waingereza wanasema Public enemy. Hawataki kumuona na wako ambao wametishia hata kumtoa roho.
Haraka msafara wa Colombia uliongezewa ulinzi baada ya kusambaa haraka kwa taarifa hizo na zile za Neymar kusafirishwa kwa helkopta hadi Sao Paulo ambako anatibiwa na baadaye atakwenda kupumzika nyumbani.

Wabrazil kadhaa walisafiri hadi kwenye hoteli waliyofikia Colombia, ingawa hawakuweza kukaribia lakini waliimba na kumkashifu.
Tayari Zuniga anayekipa Napoli ya Italia ameomba radhi, lakini ndiyo amesababisha gumzo kubwa na wengi wanaamini alifanya makusudi wakitumia kigezo cha faulo nyingine aliyoifanya siku hiyo.

Zuniga alimrukia mshambuliaji wa Brazil, Hulk wakati akiambaa na mpira. Mguu wake ulikwenda moja kwa moja kwenye goti. Mashabiki hao wanasema Zuniga alipania kumuumiza mchezaji yoyote wa Brazil.

Baadhi wameweka picha za mtu akichomwa moto na kuwataka mashabiki wa Brazil popote walipo kummaliza beki hiyo, lakini wengine wameweka picha za vijana wakiwa na bunduki na kusema Colombia wamezoea vurugu na vita na wanashauri Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuwaondoa ili waingie kwenye mashirikisho ya wapiganaji kwa kutumia silaha, kama yatakuwepo.
Ukiangalia kwa makini katika faulo alizocheza kupitia video, zinaonyesha kuna walakini na huenda Zuniga alipania kufanya jambo ambalo si zuri, kweli.

Faulo ya Hulk:
Hulk alikuwa amekimbia na kuudokoa mpira hata kabla ya Zuniga kuruka, lakini anaonekana akiwa ameamini mpira ule hawezi kuuwahi na kilichobaki ni kucheza na mwili wa mshambuliaji huyo.
Kweli Zuniga anaruka mguu wake ukiwa umelenga goti la Hulk, anafanikiwa kumpata lakini bahati nzuri hajaumia kama ilivyo kwa Neymar.

Faulo Neymar:
Inawezekana Zuniga hakujua kiasi gani atamuumiza nyota huyo wa Brazil, lakini hakuna ubishi alijua anakwenda kufanya madhambi na si kuchukua mpira.
Zuniga alikuwa nyuma ya Neymar ambaye aliuficha mpira mbele yake, kwa kuwa alikuwa amegeukia kwenye lango lao, Zuniga alitakiwa kutumia akili kumpokonya mpira au kumpa presha auotoe.
Yeye akamrukia moja kwa moja na hata wakati Marcelo na James Rodriguez wakijaribu kumsaidia, Zuniga aliendelea na mambo yake kama vile hana habari.
Hoja ni hivi, wakati Colombia ilikuwa nyuma kwa bao moja, si lahisi mchezaji kufanya faulo ya kipuuzi kama ile ya Zuniga, badala yake kwa dakika tatu zilizobaki, alikiwa kupambana kuupata mpira bila kufanya madhambi ili washambuliaji na kusawazisha!
Picha:
Picha ya tukio ambalo Zuniga anamrukia Neymar mgongoni na kumvunja mfupa mdogo wa uti wa mgongo, ndiyo imeangaliwa zaidi kwa saa 24 baada ya tukio.

Awali picha iliyokuwa kiburudisho zaidi ni ile ya Robin van Persie wa Uholanzi akifunga bao kama vile anapaa, ilikuwa mechi dhidi ya Hispania.
Picha ya Zuniga na Neymar imeangaliwa na mashabiki wanaokosiwa kufikia milioni 55, wakati ile ya van Persie iliangaliwa na mashabiki milioni 48, ndani ya saa 24.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic