September 10, 2014


Mshambuliaji nyota wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Mrisho Khalfan Ngassa, amefunguliwa kesi ya madai ya talaka namba 30/2014, katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na mkewe Latifa Abdul Fundi.


Ngassa amefunguliwa kesi hiyo akidaiwa kumtelekeza na kumnyima matunzo ya ndoa mke wake tangu Juni mwaka 2011, migogoro ilipoanzia.

Kesi hiyo iliyoanza kuunguruma Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata), Kitengo cha Mashauri ya Ndoa, mambo yalikwenda ndivyo sivyo kufuatia Ngassa kutotoa ushirikiano katika baraza hilo.

Baada ya baraza hilo kushindwa kesi hiyo, liliihamishia mahakamani hapo ambapo juzi (Jumatatu), mchezaji huyo na mkewe walitakiwa kupanda kizimbani mbele ya hakimu waliyepangiwa, Timothy Lyon, lakini Ngassa alishindwa kutokea kutokana na majukumu aliyokuwanayo kwenye timu ya taifa iliyokuwa nchini Burundi.

Kufuatia udhuru huo, Hakimu Lyon aliiahirisha kesi hiyo mpaka Septemba 30, mwaka huu ambapo Ngassa na Latifa wanatakiwa kupanda kizimbani katika shauri hilo.

Katika kesi hiyo, Latifa anamdai, Ngassa talaka pamoja na mgawanyo wa mali walizochuma wakiwa katika ndoa yao ikiwemo nyumba mbili, moja iliyopo Yombo na nyingine Tegeta Basihaya jijini Dar es Salaam.

Kiwanja kimoja kilichopo Tegeta Basihaya jijini, gari aina ya Toyota Cresta, vitanda viwili, kabati dogo la vipodozi, seti ya masofa, meza, pasi ya umeme, majiko mawili ya kupikia, televisheni, redio kaseti, brenda na draya.

Pamoja na mali hizo, Latifa anamdai Ngassa ampe pesa taslimu shilingi laki mbili na nusu (250,000/) kila mwezi, tangu Juni 2011, mpaka siku ya hukumu ambazo ni kwa ajili ya matunzo tangu alipositisha kumhudumia.

Jalada la kesi hiyo liliambatanishwa na cheti cha ndoa kinachoonyesha wawili hao walifunga ndoa Mei Mosi, mwaka 2009, mashahidi wakiwa Imani Madega na Saidy Rashid.


 SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic