Naibu Waziri wa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, leo amekutana na uongozi wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na ule wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na kuagiza
kusitishwa kwa zoezi la ukatwaji wa asilimia 5.
TFF iliiagiza bodi kukata
asilimia 5 ya fedha za klabu kutokana na udhamini wa Vodacom na Azam TV, halafu
ziwekwe kwenye akaunti yake ili zitumike kwa maendeleo ya soka.
Lakini katika mkutano wa
leo, Nkamia amewasisitiza TFF, Bodi ya ligi na klabu kukutana, halafu
kulijadili hilo suala.
TFF wametakiwa kukutana kwa
pamoja na wadau hao, halafu wafikie mwafaka kabla ya kurejea serikalini.
“Wanatakiwa wakutane,
wazungumze na kukubaliana na siku nzuri ya kufanya hivyo nimeona ni Jumamosi.
“Baada ya hapo
watakachofikia mwafaka, basi watarudi serikalini na sisi tuangalie, lakini
suala la kukata fedha hizo kweli nimesitisha na sasa liangaliwe hilo la
kukutana kwanza,” alisema Nkamia ambaye kitaaluma ni mwanahabari.
Mkutano huo unasubiriwa kwa
hamu kwa kuwa pande zote tatu zimekuwa na msimamo wa aina mbili.
Bodi ya ligi pamoja na
klabu hizo za ligi kuu, zimesisitiza haziwezi kukubaliana na hilo la kukatwa
fedha zao za udhamini kwa kuwa mikataba ya Vodacom na Azam Tv iko wazi na
haielezi hilo la asilimia tano.
Lakini tayari TFF kupitia
Rais wake Jamal Malinzi ilishatangaza suala hilo halitakuwa na mjadala na
lazima wakatwe.
Pia kwa hesabu za kawaida,
inaonyesha TFF inachukua fedha nyingi zaidi kuliko hata klabu moja moja kupitia
udhamini wa Vodacom na Azam TV.
0 COMMENTS:
Post a Comment