Na Saleh Ally
TARATIBU Brazil inaanza
kusahau machungu ya kupoteza kwa idadi ya mabao 7-1 dhidi ya Ujerumani katika
mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia.
Michuano hiyo mikubwa
ilikuwa inafanyika kwenye ardhi ya Brazil ambayo ilikuwa inahitaji ushindi ili itimize ndoto ya kwenda fainali,
ikashindikana.
Maumivu makubwa zaidi
yakawa kwenye kipigo hicho, taifa likazizima, lakini hakuna lisilopita ingawa
halitapotea kwenye historia ya soka la Brazil.
Wabrazil walijua litapita
lakini haiwezi kuwa lahisi, wameanza kulifanyia kazi taratibu ikiwa ni pamoja
na kumuondoa Kocha Fellipe Scolari, kwa mara nyingine wakamuamini Dunga.
Tokea amerejea, Dunga ameiongoza
Brazil mechi tatu bila ya kupoteza hata moja, huku akishinda zote mfululizo.
Hii ni furaha, raha na
taratibu imani ya Wabrazil inarejea, pia inaondoa hisia kuwa ndiyo mwisho wa
nchi yao kutamba kisoka ulimwenguni.
Pamoja na hivyo, mabadiliko
kadhaa aliyoyafanya Dunga yameonyesha ujasiri, mfano kumrejesha Kaka kwenye
kikosi hicho, lakini kumteua mshambuliaji Diego Tardelli Martins.
Tardelli si mgeni kwa
Wabrazil wapenda soka, anakipiga katika klabu ya Atletico Mineiro ya Brazil,
anajulikana kwa staili yake ya ushambuliaji kama mtu anayewamaliza adui kwa
bastola mbili mikononi mwake, huku akipiga “pa, pa, papapapa”.
Ndoto kuu ya Tardelli
ilikuwa ni kuichezea Brazil, mara baada ya Dunga kumrejesha, amekuwa dawa mpya
ya kuhakikisha urejeshaji wa matumaini ya Wabrazil kuwa huenda mambo yako
sahihi.
Kwamba ushindi wa mechi
mbili zilizopita, moja ikiwa ni dhidi ya Colombia, si wa kubahatisha, badala
yake Brazil imerejea tena kwa kuichapa Argentina kwa mabao 2-0 katika mechi ya
kirafiki iliyokuwa inasubiriwa ka hamu ulimwenguni kote na ilichezewa nchini
China, pia kombe likatolewa.
Tardelli alifunga mabao
yote mawili yaliyoizamisha Argentina na sasa ndiye mjadala kama kweli ni sahihi
kuvaa jezi namba tisa iliyowahi kuvaliwa na wakali kama Ronaldo.
Wengi wanaona ni sahihi
ukilinganisha na Fred ambaye alionekana kutokuwa msaada hata kidogo kwa Brazil.
Uwezo aliounyesha Tardelli
katika mechi hizo mbili umekuwa gumzo lakini raha zaini ni mabao yake mawili
yalivyobadili upepo wa Brazil.
Brazil imeona imejikwaa sehemu,
ilipoanguka haikuangalia ilipoangukia, badala yake ilipojijwaa na sasa
mabadiliko madogo yanaanza kurudisha imani upya na hasa kutokana na timu
kufanya vizuri.
Brazil imeamua kurekebisha
kosa la miezi kadhaa iliyopita na sasa mambo yanaonekana kwenda sawa.
Tanzania ina kosa la tokea
miaka 34 iliyopita, lakini halina dalili ya marekebisho au harufu ya mafanikio!
Timu ya taifa, Taifa Stars
ilishiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika mwaka 1980, hadi leo haijapata
nafasi hiyo, angalau kidogo TFF chini ya uongozi wa Leodeger Tenga ilipokwenda
kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan)
mwaka 2009, kule Ivory Coast.
Ukiachana na hiyo angalau,
juhudi za kumaliza tatizo hilo sugu na maumivu makubwa kwa Tanzania,
hazionekani.
Viongozi wengi wanaoingia
madarakani ni aina ya wale wanaotaka kutetea maslahi yao tu, wasiojali wala
kuumizwa na historia inayoubana moyo wa Kitanzania katika kupenda soka.
Tanzania kupitia TFF,
inaendeleza malumbano, kuwaza mipango ya kuwafungia watu kupitia kamati zake
zenye lengo la kukomoana na kila anayekosoa ni adui.
Brazil walikubali
kukosolewa, wakakiri, wakafanya mabadiliko na sasa wanaonekana kutengeneza njia
nzuri kutoka kwenye kosa.
Miezi kadhaa tu baada ya
kuharibikiwa, sasa wanaonekana kuvuka kuingia upande wa pili kwenda
kujirekebisha huku wakiwaamini hata ambao hawakuaminiwa kama Tardelli ambao
sasa ndiyo suluhisho la safu ya ushambuliaji ya timu yao ya taifa.
Tanzania inalia miaka 34,
inapambana kupata nafasi hiyo miaka nenda rudi na walio madarakani sasa ni
afadhari ya jana. Ushirikiano hakuna, mapenzi ya kufanya kazi pamoja kwa ajili
ya utaifa yamekufa na soka linaongozwa na wengi wasiojua lolote.
Brazil wameweza kurekebisha
mambo na maumivu ndani ya siku chache tu. Tatizo wameshindwa na wanazidi
kuongeza maumivu huku ‘midomo’ ikitawala kwa kutembea zaidi kuliko ‘mikono’ kwa
ajili ya utendaji.
Nani ataiokoa Tanzania?
Ukisema uongozi wa sasa wa TFF, jibu litakuwa ni kosa kubwa. Kama si wao,
atatokea wapi wa kuanzisha mipango kama ya Wabrazil baadaye wapatikane akina
Dunga ambao watawatafuta watu kama Tardelli.
Watu hawaaminiani,
hawapendani na ajabu hawashirikiani lakini wanataka Tanzania icheze Kombe la
Mataifa Afrika! Haya ni maajabu na ikiwezekana, miaka mingine minge ya hadithi
ileile imewadia sasa kukamilisha majonzi na maumivu ya miaka 28 iliyopita, huku
wengine wakijifaidisha wao na rafiki zao kupitia soka yetu.
Kwa wanaoumia, Brazil
kupitia Dunga kwenda kwa Tardelli ni mfano sahihi wa kubadili gia na
kutengeneza imani upya kwa Watanzania na hasa kwa kushirikiana, si kutafutana
uchawi, uadui, kutishana huku wahusika wakijua tatizo ni tamaa zao na uzoefu
mdogo katika masuala ya soka.
Ni aibu kwa mtu anayejiita mwandishi wa habari kuiringanisha Brazil na Tanzania katika soka,ongea lingine Saleh hilo ni pumba za mtama!
ReplyDeleteWe Saleh rafiki yako Ndumbaro ndio basi tena!
ReplyDeleteWajanja wameshamfungia kushiriki mambo ya soka kwa kipindi cha baleh(miaka saba bila ubishi!)
sasa unasubiliwa wewe nawe upigwe nyundo ya uandishi wa michezo!
Chezea Wambura wewe!