Na Saleh Ally
Mshambuliaji Mbwana Samatta anaondoka TP Mazembe ya DR
Congo na hii si hadithi tena, Meneja wake, Jamal Kisongo amethibitisha hilo.
Awali, taarifa zilizolifikia gazeti hili na
kufanya uchunguzi kwa wiki mbili, zilionyesha Samatta alikuwa anawaniwa na timu
tatu za Ulaya, mbili kutoka nchini Ufaransa, tena zinashiriki ligi kuu nchini
humo League 1.
Lakini jana, Meneja wake, Jamal Kisongo
akathibitisha hilo kwa kusema tayari wamekuwa na mazungumzo marefu na uongozi
wa TP Mazembe na mmiliki wake, bilionea Moise Katumbi amekubali kutoa ruhusa.
“Yalikuwa mazungumzo ya kina na marefu
kiasi, lakini mwisho tumefikia mwafaka kwamba Samatta anaondoka TP Mazembe na
anakwenda Ulaya.
“Kumekuwa na mtikisiko mkubwa ndani ya
Mazembe, wengi hawakutaka aondoke. Lakini mkataba tulioingia mwanzo umembana
Katumbi, amekubali Samatta aondoke Mazembe,” alisema Kasongo, akionyesha
kujiamini.
Kasongo ambaye aliongozana na Samatta hadi
Lubumbashi, DR Congo ambako aliingia mkataba na timu hiyo kwa mara ya kwanza,
amesema hadi mwezi ujao kitakuwa kimeeleweka.
“Suala la kuwa majeruhi ndiyo
limemchelewesha Samatta, lakini atalazimika kusubiri wiki tano alizopewa na
daktari. Ndiyo maana nilizuia asirudi Mazembe, sikupenda atumike angeweza
kuumia tena.
“Anatakiwa kwenda Ulaya, nisisitize si
majaribio na wakala wake ni mtu mkubwa tu nchini Ufaransa, hivyo
atalishughulikia suala hilo na kila kitu kinaenda vizuri.”
Kama ilivyo kwa kikosi cha timu ya taifa,
Taifa Stars, Samatta amekuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Mazembe na
kumekuwa kuna ugumu kumng’oa Lubumbashi hadi juhudi za Kisongo zilipozaa
matunda.
Alijiunga na Mazembe misimu mitatu iliyopita
akitokea Simba ya Dar es Salaam.
0 COMMENTS:
Post a Comment