Na Saleh Ally
HESABU ya mechi saba za
Ligi Kuu Bara ambazo Mbeya City imecheza kabla ya ligi hiyo kusimama,
zinaonyesha hazijajipanga vizuri.
City imecheza mechi saba,
imeshinda moja, sare mbili na kupoteza mechi nne, hivyo kuifanya ikusanye
pointi tano tu na sasa inashikilia mkia ikiwa imezibeba timu 13 mgongoni!
Matokeo hayo yamewapa
presha kubwa mashabiki, viongozi na wachezaji wa Mbeya City ambao kwa asilimia
95 wana kikosi kilekile cha msimu uliopita kilichoshika nafasi ya tatu.
Mbeya City ilishika nafasi
ya tatu ikiwa ndiyo imepanda Ligi Kuu Bara, ikawa kigogo ya vigogo,
ikazikomalia Yanga, Simba na Azam ingawa mzunguko wa pili ilionekana kushuka.
Mwendo mbaya, umesababisha
kocha Juma Mwambusi ajiuzulu. Mwenyewe amehojiwa redioni na kusema kuwa
ameachia ngazi, lakini uongozi bado unakwenda kulizungumzia, huenda wanjaribu
kumtuliza.
Lakini kitu kibaya zaidi,
Mwambusi amekuwa akishindwa kutoa ufafanuzi katika suala hilo, akikwepa
kuzungumza na waandishi ingawa mara moja nimemsikia akithibitisha kujiondoa.
Uongozi umekuwa ukisisitiza
kuwa, Mwambusi bado ni kocha wao, hivyo inachanganya ingawa kauli za kocha huyo
zilionyesha zimejaa jazba.
Wakati anahojiwa na Redio
One, Mwambusi alionyesha kukasirishwa na kitu na akazungumzia madai ya
wachezaji wake kuwa wapo wanaoidai timu, yeye amekuwa akijaribu kuwashawishi
wacheze kwa kujituma, lakini anaona sivyo.
Ukiangalia matumaini
yaliyojengwa na furaha ya mashabiki wa Mbeya City, tayari waliipa timu yao
daraja walilo Yanga, Simba, Azam FC kutokana na matokeo mazuri. Sasa wote
wanaona kama wanasalitiwa, ndiyo maana wamekuwa hawataki kuamini.
Ukirudi kwa viongozi,
ingawa ulikuwa ni msimu wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara, waliona mambo ni rahisi,
yanawezekana, mipangilio haina ugumu, ndiyo maana sasa wanashindwa kuidhibiti
hali hiyo kwa urahisi.
Wachezaji wengi wa Mbeya
City walikuwa ndiyo wanacheza ligi kwa mara ya kwanza. Pia waliona huenda kila
kitu rahisi na wanaweza, sasa mambo yamekuwa tofauti.
Ukweli ni hivi, kama
Mwambusi amepitisha uamuzi wa kuondoka na kwa mujibu ya nilivyomsikia redioni,
basi nitamweleza mambo mawili.
Kwanza ameondoka mapema na
pili hakuondoka kwa maana ya kwamba ameshindwa, lakini hakukubali kukaa
ajaribu, badala yake amezisikiliza hisia zake, unaweza kusema Mwambusi amesusa.
Kiongozi au baba au mzazi,
hukubali kubaki wakati laini yaani wa raha. Pia haiachi familia au timu kipindi
cha shida, au cha matatizo. Mwambusi hakuwa tayari kulaumiwa, lakini alitakiwa
kukubali ili atumie nguvu yake na uwezo wa msimu uliopita ili kuweka mambo
sawa. Lawama haziishi dunia hii, hata ufanye mazuri kama malaika.
Ukiachana na Mwambusi,
Mbeya City pia walijisahau na mtazamo wangu kuna mambo matatu yatakuwa
ymechangia kuwapa ugumu, nitawaeleza kama zawadi yao. Wakiweza wanaweza
kuyafanyia kazi.
Moja:
Wazungu wanasema ‘surprise’,
yaani kitu cha kushtukiza. Hakuna aliyejua City ingekuwa imejiandaa kama
ilivyokuwa msimu uliopita, mwanzo walionekana kama wanabahatisha, lakini
wakaendelea kusonga.
Utaona mzunguko wa pili,
watu wakatulia, wakaanza kupambana nao, ndiyo maana ilipoteza mechi zikiwemo
mbili dhidi ya Yanga na Azam FC pale Sokoine.
Pili:
Msimu huu, timu zikikutana na
Mbeya City, zinajua kuwa zinakwenda kupambana na nani na kuifunga ni zaidi ya
ushindi. Hivyo makocha na wachezaji wanajiandaa vilivyo na hiyo inaonyesha
ugumu wa kila mechi kwao.
Si kama ilivyokuwa msimu
uliopita kwa kuwa hakuna aliyejiandaa kupita kiasi dhidi yao.
Tatu:
Hili linaweza likawaudhi,
lakini nidhamu kwenye kikosi cha City imeshuka, tena hii ni hadharani kwa
vitendo. Wamekuwa wakigombana au kuwazonga waamuzi bila ya woga, ujeuri wa wazi
na huenda ni mafanikio yamewasahaulisha.
Achana na nje ya uwanja,
kuna matukio ya wachezaji hao kuteremka kwenye basi lao, barabarani na kuwapiga
madereva kisa wameziba njia. Wao si askari wa usalama barabarani, hauwezi
kusikia Cristiano Ronaldo kazozana na dereva wa lori eti kisa amelizuia basi la
Real Madrid lisipite.
Kiburi si maungwana, hakuna
aliyefanikiwa kupitia kiburi, badala yake juhudi, malengo na kuepusha kuvimba
kichwa. Jamani, matatizo yanamfanya mtu akue zaidi. Kyala awasajo.
MATOKEO:
MECHI
UWANJA
1. Mbeya City 0-0 JKT Sokoine
2. Mbeya City 1-0 Coastal Sokoine
3. Ruvu
0-0 Mbeya Mabatini
4. Mbeya City 0-1 Azam Sokoine
5. Mbeya City 0-2 Mtibwa Sokoine
6. Mgambo 2-1
Mbeya Mkwakwani
7. Stand
1-0
Mbeya
Kambarage
MSIMAMO BARA:
P W D L F A GD PTS
1. Mtibwa 7 4 3 0 10 3 7 15
2. Yanga 7 4 1 2 9 5 4 13
3. Azam 7 4 1 2 8 4 4 13
4. Coastal 7 3 2 2 9 7 2 11
5. Kagera 7 2 4 1 6 4 2 10
6. JKT 7 3 1 3 7 7 0 10
7. Simba 7 1 6 0 7 6 1 9
8. Polisi 7 2 3 2 6 7 -1 9
9. Mgambo 7 3 0 4 4 7 -3 9
10. Stand 7 2 3 2 5 9 -4 9
11. Ruvu 7 2 1 4 4 7 -3 7
12. Prisons 7 1 3 3 6 7 -1 6
13. Ndanda 7 2 0 5 8 13 -5 6
14. Mbeya 7 1 2 4 2 6 -4 5
0 COMMENTS:
Post a Comment