Ili kuhakikisha timu yake
inapata ushindi wa mabao mengi, Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Puijm
amewataka washambuliaji wake Mrundi, Amissi Tambwe na Mliberia, Kpah Sherman
kupiga mashuti wanapofika mita 20 kutoka kwenye lango la wapinzani.
Kocha huyo hadi kufikia leo
Jumamosi anakuwa ametimiza siku saba tangu aanze kibarua cha kukinoa kikosi
hicho akimrithi Mbrazili, Marcio Maximo.
Timu hiyo, hivi sasa ipo
kwenye maandalizi kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC
itakayochezwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha huyo, alionekana
akitoa maelekezo ya kupiga mashuti ya umbali huo wakati wa mazoezi ya timu hiyo
yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam zoezi hilo
liliwashirikisha na viungo wa timu hiyo.
Wakati timu hiyo ikiendelea
mazoezi ya hayo, kocha huyo alisikika akifoka kwa kuwaambia washambuliaji na
viungo hao kupiga mashuti, wakati mwingine alionekana akipiga filimbi
kusimamisha mazoezi hayo na kutoa maelekezo kwa wachezaji wake.
“Kuna sababu gani ya kutoa
pasi mnapokaribia kwenye goli, mnapokaribia goli la wapinzani wetu mnatakiwa
kupiga mashuti na siyo kupigiana pasi zisizokuwa na msingi.
“Tambwe na Sherman
mnatakiwa mlitambue hilo, sitaki lijitokeze tena mazoezini na kwenye mechi,
kikubwa kinachoangaliwa ni ushindi,” alisikika kocha huyo akiwaambia wachezaji
wake.
0 COMMENTS:
Post a Comment