INGAWA ilikuwa jana, lakini kheri ya sikukuu ya Krismasi tukiwa
tunaelekea mwaka mpya, nawaombea wadau wote wa safu hii ya Hoja Yangu kila la
kheri katika maisha yenu ya kila siku.
Naamini salamu zangu pia zitafika kwa wadau
wengine wa michezo na hasa wale wa soka ambao wamekuwa wakiifutilias afu hii
kwa ukaribu zaidi.
Baada ya salamu, kidogo leo ningependa
kujadili mambo kisikukuu kidogo huku nikijaribu kuangalia hawa jamaa zetu,
wenzetu na ndugu zetu, Yanga na Simba wanaojulikana kwa jina la ukongwe,
wamefanya nini?
Ukitaka kufanya tathimini kwamba Yanga na
Simba wamefanya nini tokea sikukuu ile ya Krismasi hadi mwaka mpya unaokuja,
utagundua hakuna.
Badala yake ni vitu vilevile vya mazoea
ambavyo kuanzia uongozi, wanachama hadi mashabiki ni wamemfunga nani,
wamemsajili nani, basi.
Simba wanaendelea kujivunia kwamba
wanapokutana na Yanga, wao hawafungiki. Katika misimu hii miwili wamekuwa
wakiwanyanyasa, hilo halina ubishi.
Yanga nao wanaongoza kwa kusajili wachezaji,
tena ghali, kutoka nchi mbalimbali zikiwemo hadi za Afrika Magharibi.
Simba wanaweza kusema ndiyo timu ya Tanzania
ambayo imeweka rekodi mpya tokea ile kanuni ya timu za Tanzania kusajili
wachezaji wa kigeni watano tu ilipopitishwa. Maana wachezaji wao wote watano,
wanatokea nchini Uganda!
Labda kunaweza kuwa na sifa ya kwamba
wamechagua viongozi wapya na wameanza kazi. Lakini nao wameingia Krismasi,
wakiwa hata hawajaanza kutengeneza uwanja wa mazoezi angalau.
Yanga ndiyo waliishaonyesha ramani, hakuna
walichofanya hadi leo zaidi ya kuelezwa mambo yataanza hivi karibuni, ramani
ipo!.
Krismasi ile, hadi hii ya jana, sasa
tunaelekea mwaka mpya, mambo yanaweza kuendelea kubaki vilevile.
Ninaamini kila Krismasi zinavyoongezeka,
tunazihesabu na kuziacha nyuma nyingine huku Yanga na Simba zikiendelea kubaki
zilizo, maana yake tunaziacha nyuma.
Mimi na wewe tunapoziacha nyuma, maana yake
dunia inawaacha nyumba watu wa Yanga na Simba na wanaendelea kuwa na maendeleo
ya Krismasi ya mwaka 1990, wakati tumeingia mwaka 2015.
Kuanza leo ni bora zaidi kuliko kusubiri
kesho. Yanga na Simba wanaweza kuwa na vitu vingi sana vya kujivunia kuhusiana
na klabu yao. Chepesi zaidi kuliko vingine ni rangi za njano na kijani na
nyekundu na nyeupe.
Hizo zitakuwa ni zao milele, hawahitaji kuzikarabati
wala kuzibadili, ndiyo mali pekee ambayo haiumizi kichwa kwao.
Lakini ukweli ni lazima kila kiongozi awe na
plani ya kujivunia kuangalia kipi amefanya baada ya muda fulani. Krismasi hadi
Krismasi ni mwaka mzima.
Kwa kiongozi yoyote mpenda maendeleo lazima
atajiuliza kuwa katika kipindi cha miezi 12 amefanya kitu gani cha kujivunia na
anatakiwa kuendelea kufanya nini.
Ninaamini viongozi wa sasa wa juu kabisa wa
Simba na Yanga hawawezi kuwa na sifa ya kutaka kufaidisha matumbo yao. Lakini
hilo nalo halitakuwa na maswali hata kidogo kama wakionyesha mwelekeo tofauti
wa maendeleo ya klabu.
Kusajili wachezaji wa nje, kuishinda timu
nyingine, yote hayo yataendelea kuwepo na kamwe hayawezi kuingia kwenye rekodi
ya maendeleo na badala yake yatabaki kwenye rekodi za uchezaji wa timu au
perfomance.
Kipimo cha kwamba kiongozi fulani aliingoza
timu kuinyanyasa Yanga au Simba wakati akiwa madarakani, halafu hakuna
maendeleo mengi, sasa imepitwa na wakati.
Simba na Yanga zinapaswa kuendana na ukubwa
wa historia yao badala ya kuwa na mwili mdogo halafu zinalazimisha kuvaa nguo
kubwaaaaa!
Hivi kwanini viongozi hawa wa simba hawataki kuuendeleza ule uwanja wa bunju ambao Rage alishawaonyesha njia ?mi nilidhani pale ndio wangeanzia kwa kuwa mwenzao alipigana sana kuhakikisha anafanya ambacho kiliwashinda viongozi karibu wote waliowahi kuiongoza simba.japo hii haisemwi lakini ndio ukweli,rage na mapungufu yake yote ya kibinadamu lakini alionyesha njia,viongozi waliopo madarakani waifuate hiyo njia angalau kwa kuweka magoli tu kwenye ule uwanja
ReplyDelete