Kikosi cha Yanga kiliwasili salama Kisiwani
Zanzibar, jana, huku kikimuacha nyota wake Danny Mrwanda jijini Dar baada ya
kukosa tiketi, lakini kubwa zaidi ni kitendo cha uongozi wa timu hiyo kugomea
hoteli walizoandaliwa na Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA).
Yanga ambayo ipo visiwani humo kwa ajili ya
Kombe la Mapinduzi ambalo limeanza jana, ililazimika kuwasambaza wachezaji wake
katika hoteli mbalimbali kutokana na kukosa hoteli ya kukaa pamoja.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano wa Yanga,
Jerry Muro alisema wameshindwa kukaa kwenye hoteli walizoandaliwa na waandaaji
wa mashindano hayo kutokuwa na hadhi kutoendana na klabu yao.
“Hoteli ambazo walitupa hazikuendana na hadhi
yetu, tukaamua kutafuta wenyewe nyingine, lakini nyingi tukakuta zimejaa,
nafikiri hii inatokana na shughuli ya mapinduzi inayoendelea kisiwani hapa,
hivyo wachezaji wamesambaa katika hoteli tofauti huku tukiendelea kutafuta hoteli
moja ya kukaa wote,” alisema Muro.
Kuhusiana na ishu ya Mrwanda, ofisa huyo
alisema Kocha Hans van Der Pluijm alitaka kusafiri na wachezaji wote lakini ZFA
wakatuma tiketi za wachezaji 21, hivyo Mrwanda akabaki Dar lakini anatarajiwa
kujiunga na wenzake leo Ijumaa.
0 COMMENTS:
Post a Comment