Azam FC imeondoka
nchini jana, Saa 2:30 Usiku kwa
Ndege ya Shirika la Kenya (Kenya Airways) kuelekea nchini Sudan tayari kwa kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Ligi
ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merreikh.
Azam wanaondoka wakiwa na
pigo kwa kuwa watawakosa wachezaji wao mahiri watatu Kipre Balou, Mudathir
Yahaya na Wazir Salum ambao wana matatizo tofauti.
Usajili wa Mudathir
unaonekana kuwa na matatizo huku Kipre na Salum wakisumbuliwa na majeraha.
Mechi ya mabingwa hao wa
Tanzania Bara itapigwa Jumamosi saa 2 usiku.
Huu utakuwa mchezo wa pili
kwa timu hizo kukutana baada ya awali kuvaana kwenye Uwanja wa Chamazi na
vijana hao wa Tanzania wakaibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Katibu wa Azam FC, Idrissa Nassor amesema kuwa kikosi cha timu hiyo
kimeondoka nchini jana na wachezaji 21, huku wengine watatu wakishindwa
kuondoka kutokana na kuwa na matatizo tofauti.
“Timu inatarajia kuondoka leo (jana), saa mbili usiku kwa
Ndege ya Shirika la Kenya, kuelekea Sudan ambapo tutaondoka na wachezaji 21
kati ya 24, tuliowasajili ambapo watatu kati yao hawatakwenda kutokana na
matatizo mbalimbali.
“Kuhusu Kavumbagu, paspoti
yake ilikuwa imejaa hivyo alilazimika kurejea kwao Burundi kuirekebisha, tayari
amesharejea na atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokwenda.
“Tumejiandaa vizuri na kitu
chochote kitakachotokea kwani na sisi tuna akili timamu kama kuna hujuma yeyote
ile ambayo itatokea tutajua jinsi ya kukabiliana nayo,” alisema Nassor.
Tunaomba Mungu awaepushe na maovu yao,tunawaombea ushindi tena.
ReplyDelete