February 25, 2015


Na Saleh Ally
MCHEZO wa ngumi ni wa pili kwa ukubwa au umaarufu hapa nyumbani Tanzania, lakini hakuna anayeweza kukataa ndiyo mchezo wenye wanamichezo wengi sana masikini!


Kuna maswali mengi ya kujiuliza ni kwa nini, lakini hali halisi inaonyesha na mfumo unaouendesha mchezo huo unathibitisha mapema kwamba kama itaendelea hivyo, huenda hali hiyo ikabaki hivyo milele.

Ajabu kama itakuwa hivyo kwa kuwa kuna mambo mengi yaliyotendeka hivi karibuni yanaonyesha utajiri uliopo katika mchezo wa ngumi, unaweza hata kuufananisha na utajiri wa madini, nitafafanua.

Mabondia wawili nyota duniani, Floyd Mayweather na Manny Pacquiao watakutana katika pambano kali Mei 2, mwaka huu. Wao wawili tu, watalipwa jumla ya dola milioni 250 (zaidi ya shilingi bilioni 425), hii ni rekodi mpya.


Mayweather ambaye hajapigwa hata mara moja katika mapambano 47, atachukua dola milioni 150 (zaidi ya Sh bilioni 225) na Pacquiao ataondoka na dola milioni 100 (zaidi ya Sh bilioni 170), usisahau hilo ni pambano moja tu.

Achana na hilo, Jumamosi iliyopita imefanyika biashara katika Jiji la New York, Marekani. Glavu nne, mbili alizovaa gwiji, Mohammed Ali na mbili alizovaa, Sonny Liston siku hiyo akipigwa na Ali zimeuzwa kwa kitita cha pauni 622,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.5).

Nakukumbusha, pambano hilo lilifanyika Ukumbi wa American City of Lewiston, Maine nchini Marekani. Ali alishinda katika raundi ya kwanza kwa ngumi kali iliyopewa jina la ‘Phantom punch’.

Angalia, miaka 50 baadaye, glavu nne walizovaa wanaume hao zinauzwa kwa kitita cha zaidi ya Sh bilioni 1.5. Hii ni heshima kubwa na sehemu ya kuonyesha kiasi gani mchezo wa ngumi ulivyo na nguvu na biashara kubwa.


Utasema hiyo ni Marekani, lakini ukweli katika nchi nyingi mabondia ni matajiri, tena kwa kucheza mechi tatu hadi nne kwa mwaka. Hapa nyumbani wako wangeweza na tuna mifano kidogo, nitakukumbusha.

Wakati wa akina Matumla, anza kwa Rashid, alijenga nyumba mbili au tatu, alimiliki magari likiwemo Mercedes Benz. Mdogo wake Mbwana naye alijenga nyumba.

Usisahau hata Francis Cheka ambaye biashara yake ni kuokota chupa, leo amejenga na anaitwa “baba mwenye nyumba” kwa ajili ya ngumi.

Walipofikia kina Matumla na Cheka, ilikuwa ni hatua fupi kabisa lakini ukweli mchezo wa ngumi umetawaliwa na viongozi wabinafsi, mabondia wasiopendana na mapromota wengi ni matapeli.

Hao wameufanya mchezo uishie ulipo sasa, Cheka yuko gerezani kutokana na kumpiga meneja wake wa baa. Amefikia huko kwa kuwa hakuwa na meneja, angejitambua yeye ni nani, kazi ya kusimamia angemuachia meneja wake, huenda angemkwepa ‘shetani’.

Kamati iliyoundwa kumkomboa gerezani imevunjwa, Rais wa Oganaizesheni za Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah ‘Ustaadh’ amesema haikuwa na watu ‘wakweli’. Hii ni picha ya kuonyesha watu wa ngumi wakoje, ukweli ni sawa na kusema tuko makaburini tayari kuuzika kabisa mchezo huo nchini.

Familia ya akina Matumla imetitia, Mkwanda Matumla na kaka yake Mbwana walikamatwa wakiwa na madawa ya kulevya. Hadi leo Rashid Matumla amekuwa akihaha kuwasaka wadogo zake bila mafanikio, hakika anatia huruma.

Wadau wa mchezo wa ngumi mnaweza kukataa haya ninayosema, lakini leo nataka niwaambie ukweli bila kona, kwanza kabisa hamjitambui na mnatumiwa na wajanja wachache.

Lakini pia hamjifunzi kuwa mchezo huo ni mkubwa, mchezaji anaweza kuwa tajiri hata kuliko kuuza unga, akawa maarufu na kuishi maisha ya juu kama atajipanga vema.

Wanaosimamia mchezo huo nao ni tatizo, wakija watu makini viongozi wa mashirikisho wanawaangusha makusudi.

Lakini mabondia nao ni tatizo kubwa. Hawaangalii hata hatua moja mbele. Wanatumiwa wao kwa wao 
kumalizana wenyewe na kuwafaidisha wengine. Amkeni jamani, mko mgodini lakini wanaochimba ni wale wanaotokea kwa jirani ambako hawana machimbo, mtatumiwa hadi lini? Mtashituka lini ili mjitambue?
Hali hii imekuwa inaudidimiza mchezo huo na matokeo yake kutoka kwenu, hadi watoto wenu wamekuwa wakirithi, badilikeni. Mweh!



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic