February 5, 2015


Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetoa adhabu kwa watu tisa wakiwemo viongozi, wachezaji na kocha mmoja kwa kupatikana na hatia ya makosa ya kinidhamu.


Katika kikao chake kilichofanyika juzi (Februari 3 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Kamati hiyo imewafungia mwaka mmoja viongozi wawili wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) Mkoa wa Mwanza kwa kuwashawishi wachezaji wa Mwanza Queens kugomea uamuzi halali.

Sophia Tigalyoma (Mwenyekiti) na Katibu wake Hawa Bajanguo walitiwa hatiani kwa kuwashawishi wachezaji kugomea uamuzi wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF kutupa rufani yao dhidi ya Kigoma.

Kocha wa Polisi Tabora, Eliakim Christopher amefungiwa mechi kumi na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 39(2) ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kutiwa hatiani kwa kumtukana refa wakati wa mechi kati ya timu yake na Panone FC iliyochezwa mjini Moshi.

Wachezaji wa JKT Oljoro FC, Dihe Makonga, Swaleh Idd Hussein, Ramadhan Mnyambegu na nahodha Shaibu Nayopa wamefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kuzingatia kanuni ya 36(10) ya FDL kutokana na kufanya vurugu kwenye mechi kati yao na Burkina Faso iliyochezwa mjini Morogoro.

Mtunza Vifaa (Kit Man) wa JKT Oljoro FC, Eliud Mjarifu amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi kati ya timu hizo iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Pia Mjarifu amepewa onyo kali na kutakiwa kutorudia tena kutenda kosa, kwani hata mwenendo wake wakati wa shauri hilo ulionyesha utovu wa nidhamu mbele ya Kamati.

Naye Mtunza Vifaa wa Rhino Rangers FC, Albert Mbuji amefungiwa miezi sita na faini ya sh. 200,000 kwa kupatikana na hatia ya kuwatukana na kugomea uamuzi wa marefa kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma. Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 40(2) ya FDL.

Kamati ilikubaliana na utetezi wa Gunda kuwa, jukumu la timu hiyo lilikuwa mikononi mwa viongozi wa TWFA Singida, na tayari SIREFA kupitia Kamati yake ya Nidhamu ilishatoa adhabu kwa viongozi wa timu hiyo kutokana na kitendo hicho.

Nayo malalamiko ya Polisi Tabora FC kutaka mechi yao dhidi ya Toto Africans FC irudiwe kwenye uwanja huru (neutral ground) kwa madai ya kuchezeshwa zaidi ya muda unaotakiwa, na kutokuwepo ulinzi wa kutosha kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza yamekataliwa.

Pia Kamati ya Nidhamu imeelekeza malalamiko ya timu za Mwadui FC na Polisi Mara FC dhidi ya Toto Africans kwa kumchezesha mchezaji Ladislaus Mbogo bila kuonyesha leseni yake yasikilizwe haraka na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa vile si ya kinidhamu.

Wakati huo huo, Kamati ya Nidhamu inaendelea na kikao chake leo (Februari 5 mwaka huu) kusikiliza malalamiko mengine ya kinidhamu yaliyofikishwa mbele yake.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic