February 13, 2015


Na Saleh Ally
Yanga ilizaliwa mwezi huu, mashabiki wa Yanga wanajua kuwa wapo katika mwezi muhimu kwa kuwa ndiyo kipindi ambacho klabu yao pendwa ilianza kuhesabika.


Februari 12, 1935, Yanga ikawa hewani. Ndiyo maana ni sahihi kusema tayari klabu hiyo imetimiza miaka 80.

Hakuna ubishi tena kwamba Yanga iliyoanza kwa jina la New Youngs, ndiyo klabu kongwe nchini na huenda ndiyo jambo kubwa zaidi wanachama na mashabiki wake wanaweza kujivunia. Simba imetokea ubavuni mwake, hali kadhalika Pan African na zote zinajulikana kama klabu kongwe.

Katika mitandao mbalimbali ya kijamii, mashabiki na wanachama wa Yanga kutoka sehemu mbalimbali nchini na nje ya mipaka ya Tanzania, wamekuwa wakisherehekea klabu yao kufikisha umri huo mkubwa.

Nilisikia baadhi ya wanachama na mashabiki hao walikuwa katika maandalizi kwa ajili ya kufanya sherehe za miaka hiyo ya kuzaliwa kwa klabu yao.

Wana haki ya kufurahia umri mkubwa lakini najaribu kujiuliza, kwa miaka au umri wa Yanga na ilichonacho sasa ni sawa kushangilia au ni bora kuweka ‘msiba’?

Yanga inategemea mapato yake, inategemea kujiendesha kupitia soka, unaweza kusema uhai wa klabu hiyo ni soka? Lakini katika umri wa miaka 80, haina hata uwanja wa mazoezi!

Yanga yenye miaka 80, yaani 40 mbili au 20 mara nne, haina timu ya vijana ya kueleweka. Haina chumba kwa ajili ya kuweka kumbukumbu zake, Wazungu wanasema museum. Ungeweza kuona makombe na picha za wakongwe, viongozi waliopita na mambo mengine.

Hata makao makuu ya klabu, mazingira ni mabaya, ya hovyo kabisa na huenda viongozi wakasikia vibaya kuambiwa kwa kuwa kweli panatia aibu!

Ukiachana na mpira, pamoja na ukubwa wa Yanga, klabu hiyo haina biashara nyingine yoyote iwe ya kuuza jezi, vibeba ufunguo, kofia, mipira, bendera na vitu vingine, ipo tu ili mradi.

Yanga kama klabu, ingeweza kujivunia migogoro, kutopendana, watu kufanyiana majungu, kusengenyana, unafiki na mengine ambayo si ya maendeleo.

Ukiwa muungwana tulia, tafakari uone kama kweli Yanga ina kitu kikubwa cha kujivunia zaidi ya rangi zake mbili, kijani na njano na ndiyo kitu namba moja mashabiki wake wanaweza kukitanguliza mbele yao kwa mafanikio makubwa.

Yanga haijafanya vizuri michuano ya Caf, hauwezi kuifananisha na TP Mazembe, Enyimba, El Merreikh, Al Ahly, Zamalek na timu nyingine kongwe za Afrika.

Yanga ilipata maendeleo makubwa katika miaka ya 1970 na 1980 baada ya hapo, mafanikio yake ni ya hadithi zaidi kuliko vitu vinavyoonekana.

Angalia majengo yake mawili, lile la makao makuu, makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga na lile la Mtaa wa Mafia jijini Dar es Salaam, yalijengwa na kina babu.

Tangu waliopo ambao unawaita vijana waanze kuongoza klabu hiyo mwishoni mwa miaka ya 1990 na sasa ya 2000, hawana jengo au kitega uchumi chochote kilichoongezeka na hata yale majengo waliyoachiwa, mfano Uwanja wa Kaunda, yamechakaa.

Waliopo kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 2000, ni wale wanaoweza kutunza rekodi nyingi katika makaratasi na si utendaji. Walio na mipango mingi isiyotekelezeka.

Hivyo kuliko Yanga kukutana na kufanya sherehe ya kufurahia kutimiza miaka 80, vema wangekutana na kufanya ‘msiba’ wa kutathmini kuwa pamoja na kufikisha umri huo, wana nini cha kujivunia?


Hadi wanafikisha miaka hiyo, tangu waliokuwa wakijulikana kama vijana waanze kuchukua klabu, wamefanya nini, kipi wanacho cha kujivunia, wapi wameteleza, nini cha kufanya, wapi wabadili gia? Kama wakiona sherehe ndiyo sahihi, maana yake wameridhika kusherehekea miaka 100 wakiwa hapo walipo.

1 COMMENTS:

  1. Sawa Saleh sasa tutafanya bethidei ya simba hapo mwakani,tutakualika mwanachama wetu ila TFF hatuwataki kwani wamezidi kutuwekea ngumu wanalunyasi!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic