Pamoja na Yanga kuendeleza wimbi la
ushindi katika michezo yake, nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
bado ameendelea kumfikiria mshambuliaji wa BDF XI ya Botswana, Kobelo
Seakanyeng kwa kuwa alimpa wakati gumu kwenye mchezo wa awali.
Yanga ambayo ilifanikiwa kuibuka na
ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu hiyo katika mchezo wa kwanza wa Kombe la
Shirikisho dhidi ya Waswana hao jijini Dar, Ijumaa hii itarudiana nao nchini
kwao na Cannavaro bado anamfikiria straika huyo.
Cannavaro amesema kuwa licha ya ushindi
walioupata katika mchezo wa awali, bado amekuwa akifikiria namna ya kumkaba
straika huyo ambaye alimsumbua kwenye mchezo wa kwanza.
“Kazi kubwa bado ipo nchini Botswana
kwa sababu jamaa wapo sawa, kuna yule straika wao aliyekuwa amevaa jezi namba saba
halafu amenyoa kipara, ni mjanja halafu alikuwa anasumbua.
“Unajua amenipa muda wa kufikiria
jinsi ya kumthibiti katika mchezo wa marudiano pamoja na kucheza kwa tahadhari kubwa kwa sababu tunaenda
kucheza ugenini na kwa jinsi alivyocheza hapa, mbele ya mashabiki wao atakuwa
hatari zaidi kwetu,” alisema Cannavaro.
Yanga wanatarajia kuifuata BDF keshokutwa
Jumatano, wakiwa na timu ya watu 37.
Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Kiboroha, amesema
kati ya watu hao, 25 watakuwa ni wachezaji huku viongozi na benchi la ufundi jumla wakiwa 12.
“Mchezo
wetu utachezwa saa kumi na moja jioni siku ya Ijumaa na tumejiandaa kuona
tunafanikiwa kushinda mchezo huo na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuendelea
kusonga mbele,” alisema Kiboroha.
0 COMMENTS:
Post a Comment