March 18, 2015


Kikosi cha Yanga kimeijulia janja ya wapinzani wao FC Platinum ya Zimbabwe katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho utakaopigwa wiki mbili zijazo huko Zimbabwe, baada ya kuamua kuondoka nchini siku tano kabla kwa kile walichosema kuwa hawataki kurudia makosa ya Wakenya, Sofapaka yaliyowagharimu na kuishia kunyeshewa mvua ya mabao, huku wakisema watarejea nchini mara tu baada ya mchezo.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, Yanga itaondoka nchini Machi 29, mwaka huu ambapo mchezo wao unatarajiwa kupigwa kati ya Aprili 3 na 5.

Muro alitaja sababu mbili za kuwafuata Wazimbabwe mapema; mosi, umbali mrefu kutoka Mji Mkuu wa Zimbabwe, Harare kwenda kwenye uwanja utakaotumika, pili ni kutaka kuzoea hali ya hewa.

Muro alisema umbali kutoka Harare kwenda sehemu yenyewe ni muda wa saa 10, jambo lililowaathiri Wakenya Sofapaka na kujikuta wakitolewa kwa jumla ya mabao 4-2.

 “Sofapaka walikwenda siku moja kabla ya mchezo, wakidhani kuwa watachezea pale Harare, kumbe haikuwa hivyo.

“Umbali kutoka mji mkuu kwenda Bulawayo ni saa saba, kisha kuna safari tena ya saa tatu kufika huko mgodini (kwa Platinum), hivyo walijikuta wakifika saa nane za usiku na kucheza mechi kesho yake. Kwa hiyo tumechukua tahadhari ili na sisi yasitutokee ya Sofapaka.  Pili, tunataka wachezaji wetu wazoee hali ya hewa ya kule kabla ya mchezo,” alisema Muro.

Yanga ilitinga hatua ya kwanza kwenye michuano hiyo baada ya kuiondosha BDF XI ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2.

Wakati huohuo, Muro ametangaza kuwa, wale wanaotaka kwenda Zimbabwe kwa ajili ya kuipa sapoti Yanga, wanatakiwa kujiandikisha klabuni na si sehemu nyingine, ambapo ni lazima wawe na hati ya kusafiria (paspoti) na nauli ya kwenda na kurudi ni laki tatu.

Wakati huohuo, uongozi wa klabu hiyo umesema kuwa wataondoka nchini Zimbabwe mara tu baada ya kumalizika kwa mechi hiyo.

“Tutaondoka na kila kitu chetu, hatutaki kutumia bidhaa zao maana kwenye soka kuna mambo mengi na hasa fitna. Kwa hiyo kukwepa yote, tumeamua tubebe vyakula vyetu na maji.

“Ndiyo maana tumeamua punde tu baada ya mchezo, tutaanza safari yetu usiku huohuo baada ya mechi na kurejea nchini kutokana na mambo kama hayo ya fitna,” alisema Muro.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic