March 13, 2015


Upendo hauna sehemu fulani, mfano kwenye nyumba za ibada au ndani ya familia nyumbani kwa fulani, yeye, mke na watoto wake. Upendo ni nguzo ya mwendo wa maisha kokote kule.


Hata wanyama wanapendana na wanategemeana ili kuendesha maisha yao kwa amani. Hakuna upendo, basi hakuna amani na ikiwemo wakati hakuna amani, basi ni unafiki.

Kocha Sylvester Marsh ni mgonjwa, anasumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya koo, nimeelezwa hali yake si nzuri.

Juhudi ya kutaka kumuona nilizozifanya kwa takribani wiki sasa, zimekwama na nimeelezwa madaktari wamekuwa wakizuia kumuona kutokana na hali yake.

Nimeelezwa Marsh ni mgonjwa kwa kuwa kula yake imekuwa ni ya shida, pia kadiri siku zinavyosonga mbele, hata kumeza mate yake limekuwa ni tatizo, maneno haya nimeelezwa na mmoja wa watu wanaomuuguza.

Najua unamkumbuka Marsh, huyu aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars, Kilimanjaro Stars, pia amefundisha klabu mbalimbali ikiwemo Azam FC.

Wakati fulani niliwahi kuandika kuhusiana na msaada kwa Christopher Alex nikisisitiza kwamba wanamichezo wajitokeze kumsaidia na si kusubiri hadi mambo yaharibike.

Kuna mtu mmoja baada ya kusoma nilichoandika alisema kwamba Alex ambaye sasa ni marehemu alipaswa kujiandaa mapema ili wakati akiumwa asitegemee misaada kutoka kwa mwajiri au watu wengine.

Wala sikumlaumu, nikajua hayajamkuta, hajui ya dunia na anapaswa kujifunza kwa kuwa hajui maana ya upendo.

Si kila anayesaidiwa anakuwa hana, wakati mwingine ni vema kuonyesha upendo. Kwani wangapi wanachangiwa wakati wao wana uwezo wa kugharamia harusi zao? Hiyo ni sehemu ya kuonyesha upendo na ndiyo ubinadamu hasa.

Hatuwezi kuonyeshana upendo watu wanapokuwa na uwezo wa kusaidia au kuwaona wanafaa wakati wanapokuwa na nguvu zao na wanaweza kufanya jambo fulani ambalo litawafurahisha.

Mwenyezi Mungu ndiye anayeamua kila kitu, inapofikia akapitisha mwisho wa yoyote pia hakuna yeyote anayeweza kuzuia hilo, hili kila mtu analijua.

Pamoja na hivyo, hilo halizuii binadamu kuonyesha mlijaribu kufanya jambo kwa mpendwa wenu badala ya kusubiri mambo yamekuwa mabaya, halafu muanze kusema fulani alikuwa mtu mzuri sana na pengo lake halitazibika hata kidogo.

Kumekuwa na kawaida ya kuwapenda zaidi watu wanapoondoka. Mara kadhaa, nimekuwa nikitoa mfano huo kuhusiana nami kwamba huenda wako wengi wanaonilaumu kila siku, hawajawahi hata siku moja kusema walivutiwa na kazi yangu. Siku nikiondoka hapa duniani, wataongoza kwa kusema nilijitahidi sana.

Inawezekana kupongezana kwetu ni tatizo, kwa kuwa kila mmoja huenda alipendelea kupongezwa yeye. Basi hata kusaidiana?

Marsh anaumwa, kocha huyo ana maumivu makali, jaribu kufikiria iwapo maumivu anayoyapata yangekuwa yako? Ndiyo, inawezekana kwa kuwa nawe ni mwanadamu kama yeye pia.

Kama mlikuwa mnaona kuna juhudi zinafanyika katika kupambana kuokoa maisha ya Marsh, mimi naona bado na huenda wachache wanashiriki.
      
Kama kuna mmoja aliona imeshashindikana, basi bado tulitakiwa kuonyesha upendo wa kwamba tunapambana kwa ajili yake kwa kuwa ni mmoja wetu na kinachomuumiza sasa, kinaweza kumkuta yeyote kati yetu kwa kuwa sote ni binadamu.

Tukubali, bado hatujawa imara linapofikia suala la upendo. Kawaida rafiki sahihi, utamjua katika kipindi kigumu.

Marafiki wengi watajumuika na wewe wakati wa furaha, Marsh hana furaha, anaumia, maumivu makali nanyi mumemtenga na kukaa mbali naye, mnasubiri lini ili muonyeshe majonzi na kumjaza sifa!


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic