May 19, 2015



Tanzania imedharaulika sana! Imeonekana ni timu ya kusindikiza katika kila mashindano inayoshiriki.
Unapozungumzia katika soka, ndiyo basi kabisa. Haifai hata kidogo, lakini inaonekana kama Watanzania wamezoea vile.


Kwamba timu yao ni ya maneno tu, si vitendo. Ndiyo maana leo inafundishwa na Kocha kama Mart Nooij ambaye anaweza kuthubutu kusema yeye anawahi kunywa zake pia.

Taifa Stars, jina zuri, timu yenye wachezaji lundo wenye vipaji lakini ndiyo ambayo kila anayokutana nayo, anajipigia anavyotaka.
Nimeshuhudia Stars ikifungwa bao 1-0 na Swaziland. Timu ambayo ilikuwa ikitwangwa kila inapokutana na Stars.

Stars kama imefikia kufungwa na Swaziland na kuzidiwa kimpira, basi hakuna sababu ya kusema tuna ndoto ya kucheza Kombe la Mataifa Afrika.
Kama Stars inafungwa hadi na Swaziland, tena ikiwa na kikosi kamili, tuna lipi la kusingizia?
Angalau ingekuwa na kikosi kilichojaa vijana, tungeweza kusema mengi pamoja na kwamba tunatengeneza timu.

Lakini kipi cha kusema sasa na hasa kama utazunguzmia suala la kila huduma wanayopata kutoka kwa wenyeji wa michuano ya Cosafa pamoja na TFF.
Mimi ninaamini TFF imefanya kila kitu kwa timu hiyo pia benchi la ufundi. Lakini benchi au wachezaji wamefanya nini?

Wachezaji wanaweza kusema walifuata maagizo ya benchi la ufundi na benchi la ufundi linaweza kujitetea nini?
Kwangu ni kuhakikisha huu ni mtihani wa mwisho wa kocha Nooij. Akishindwa, basi aende zake.

Hatuwezi kuwa kichwa cha mwendawazimu huku makocha wanaoinoa timu yetu ya taifa wanashindwa kutoa matokeo.
Hakuna ubishi, wote tumeona kuwa Nooij ni kocha asiye makini na hili limejitokeza katika uteuzi wa timu.

Mimi, wewe hata TFF wameona kocha huyo alivyoteua wachezaji lundo walio majeruhi.
Nadir Haroub, Haroun Chanongo na wengine walikuwa majeruhi, lakini bado aliwateua.

Tunajua wote kocha huyo si makini, kocha huyo anafanya mzaha wakati sisi tuna ndoto ya kufanya vema.
Ni Lazima TFF iliangalie suala hilo kwa umakini, maradufu kwamba kama Stars itashindwa kuonyesha kiwango basi aende.

Cosafa uwe ni mtihani wake wa mwisho kwa kuwa hata timu zinazoshiriki sasa si za kiwango cha kutisha.

Hata katika msimamo wa viwango vya Fifa, Tanzania iko huu zaidi.
Ligi yetu ni bora zaidi ya nyingi tu. Wachezaji kama utazungumzia kiwango cha Kusini mwa Afrika, wetu ni bora na tunalijua hilo.
Wakati wa mzaha umepita, muda wa kupoteza wakati umeisha. Nooij afanye kweli, hawezi aende kwao. HAKUNA MJADALA.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic