Baada ya kufanikiwa kunasa nyota watatu, uongozi wa Klabu ya Mbeya
City, umefunguka kuwa hautafanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake na kwa
sasa wanasaka nafasi moja pekee ya mchezaji ambaye anaweza kucheza nafasi zaidi
ya moja uwanjani.
Mbeya City imefanikiwa kumnasa beki Haruna Shamte (JKT Ruvu),
kiungo Joseph Mahundi (Coastal Union) na mshambuliaji Gideon Brown kutoka Ndanda FC huku wachezaji wake wawili,
Deus Kaseke na Peter Mwalyanzi wakitua Yanga na Simba.
Katibu wa timu hiyo, Emmanuel Kimbe, alisema kuwa kwa kiasi
kikubwa kwa sasa nafasi zote zina wachezaji na wanasaka mchezaji ambaye anamudu
nafasi zaidi ya moja.
Kimbe alisema kuwa, msimu ujao vijana watapewa nafasi katika
kikosi chao, ndiyo maana hawasajili wachezaji wengi kutokana na kuwa na vijana
wenye uwezo mkubwa.
“Tumeshawasajili wachezaji takriban watatu wa nafasi tofauti, kwa
sasa tunaangalia nafasi kama moja na tunataka mchezaji mwenye uwezo mzuri na
awe anamudu kucheza nafasi zaidi ya moja, yaani kiraka.
“Lengo ni kuboresha kikosi lakini bado tuna wachezaji wengi wazuri
vijana ambao tunaamini kabisa watapambana kuhakikisha tunafanya vizuri msimu
ujao, hao tumewaongeza siyo kwamba tuna upungufu mkubwa sana,” alisema Kimbe.
0 COMMENTS:
Post a Comment