Mambo yanaonekana
kuanza kumnyoookea mshambuliaji wa Simba, Alex Masawe, ambaye anafanya
majaribio na kikosi hicho akitokea timu ya Olympic ya Afrika Kusini
inayoshiriki Ligi Daraja la Pili.
Mshambuliaji huyo
mwenye mwili uliojengeka kimazoezi, amejiunga na kikosi cha Simba tangu siku ya
kwanza katika programu ya gym, huku pia akijumuishwa katika kikosi
kilichosafiri kuelekea Tanga kwa ajili ya kujiandaa na ligi kuu.
Kocha msaidizi wa
timu hiyo, Selemani Matola, amesema mchezaji huyo ana nidhamu pia anaonyesha
juhudi kubwa katika mazoezi, lakini watautathimini uwezo wake zaidi katika
michezo ya kirafiki wanayotarajia kucheza hivi karibuni.
“Huyu ni kijana
mzuri kwa sababu ana nidhamu nzuri na anaonyesha juhudi kubwa katika programu
zetu tukiwa gym na beach. Kama akiendelea hivi, anaweza kuwa katika nafasi
nzuri ya kufuzu majaribio yake.
“Siwezi kusema
amefuzu moja kwa moja, bado tunahitaji kumuangalia katika mechi. Kwa hiyo michezo
michache ambayo tumepanga kucheza katika siku za hivi karibuni, ndiyo
itakayotoa jibu kamili juu ya hilo,” alisema Matola.
Kwa upande wake,
Massawe alisema:
“Ninafurahia
programu jinsi zinavyokwenda, kila siku unapata kitu kipya. Ninaamini nimefanya
kwa ubora katika mazoezi yetu ya kila siku. Suala la kupata mkataba linabaki
mikononi mwa makocha kwa sababu wao ndiyo wanajua umuhimu wangu katika timu,”
alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment