Zikiwa zimebaki
siku tisa kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Kagame, mshambuliaji wa Azam
FC, Mrundi, Didier Kavumbagu, amesema anatamani kukutana na timu bora katika
michuano hiyo, hasa Yanga ili kupima uwezo wake na ubora wa kikosi chao.
Yanga na Azam
ndizo timu zinazoiwakilisha Tanzania Bara katika michuano hiyo ambapo bingwa
huchota kitita cha dola 30,000 (Sh milioni 60 kwa sasa) za Kimarekani.
Azam wamepata
nafasi hiyo wakiwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, huku Yanga wakiwa wenyeji wa
michuano hiyo kwa kuwa walishika nafasi ya pili.
Kavumbagu amesema
mchezaji kujua uwezo wako ni lazima kukutana na timu yenye ubora.
“Maandalizi
yanakwenda vizuri, tumejipanga kukutana na upinzani kwa sababu mashindano
yanahusisha mabingwa wa nchi, hivyo kila timu ni bora. Ili kufanya vizuri,
tunahitaji kuwa na juhudi za ziada.
“Ninajua Yanga ni
timu bora, ninatamani sana kukutana nayo ili kupata changamoto. Unajua ili
mchezaji au timu kujua mpo imara kiasi gani, ni lazima mkutane na timu bora,
hapo ndipo mtajua mna timu ya aina gani. Binafsi ninapenda sana kukutana na
timu za aina hiyo ikiwemo Yanga yenyewe,” alisema Kavumbagu ambaye msimu
uliopita alifunga mabao 10 katika Ligi Kuu Bara.
0 COMMENTS:
Post a Comment