MICHUANO ya
Kombe la Kagame sasa imepamba moto na inaonekana hatua ya robo fainali, utamu
utazidi kunoga zaidi.
Timu ambazo
zilikuwa hazipewi nafasi kubwa sana, zimeonyesha soka safi na la kuvutia na
kuwapa wakati mgumu vigogo.
Wachezaji
waliokuwa wakipewa nafasi ya kutamba, wako ambao hawajaonyesha cheche na kuna
wengine ambao hawakuwa wakipewa nafasi wameanza kuonyesha makali yao.
Makocha ambao
waliaminika timu zao zitasonga kwa
ulaini zimekutana na ugumu wa hali ya juu, huku kukiwa na baadhi ya timu
hazionyeshi soka la kuvutia, lakini zinafanya vema.
Unaweza kusema
ni michuano ambayo ina mambo yanayoonekana, mambo yanayoweza kuwa changamoto na
pia yanayozua maswali mengi katika soka la Afrika Mashariki na Kati.
Nchi mbili za
Tanzania na Rwanda, ndiyo sehemu ambayo michuano hiyo imekuwa ikipata
changamoto kubwa na kufanya vema. Utaona mwamko wa michuano ya mwaka huu,
huenda utapaa juu zaidi kama Yanga na Azam FC zitaendelea kufanya vema.
Tatizo
ninaliona moja, wadhamini ni wachache na utaona hata zawadi za washindi
zinaendelea kuwa kidogo sana.
Bingwa
atachukua dola 30,000 (zaidi ya shilingi milioni 50). Mshindi wa pili dola
20,000 (zaidi ya shilingi milioni 35), huku wa tatu akipata dola 10,000 ambazo
ni zaidi ya shilingi milioni 18.
Fedha hizo
zinatolewa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye amekuwa akifanya hivyo kwa
zaidi ya miaka mitano sasa. Hongera kwake, jambo ambalo nimekuwa nikisisitiza
kwamba wengine wanaweza kumuunga mkono rais huyo, kabla hajachoka.
Wakati
tunaomba Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) liendeleze
juhudi kuhakikisha udhamini unapatikana na kuamsha changamoto kubwa na
ushindani wa juu zaidi, nataka nihoji kuhusu udhamini wa SuperSport.
SuperSport ni
moja ya runinga kubwa kabisa barani Afrika na duniani kote. Nimewahi kufanya
kazi makao makuu yake ya Afrika Kusini kama sehemu ya mafunzo yangu, ninaweza
kuthibitisha utajiri wao mkubwa.
Wao ni kati ya
wadhamini wa michuano hiyo na wamekuwa wakiionyesha moja kwa moja na
inawezekana ni jambo zuri kwa kuwa timu zinapata nafasi ya kuonekana na
wachezaji wanaonekana karibu Afrika kote na sehemu nyingine duniani.
Kitu pekee
ambacho ninataka kujua, udhamini huo vipi hauwezi kuzifaidisha timu kifedha?
Kwamba kabla ya zawadi, Yanga, Azam FC na timu zote zilizoshiriki michuano hiyo
zilipaswa kulipwa.
Lazima
tukubali, dunia ya sasa imebadilika, fedha za runinga ni sehemu kubwa ya mapato
katika ligi kubwa za Ulaya, Asia, Amerika Kusini na kwingineko kulipoendelea
kisoka.
Sasa vipi hapa
nyumbani, tena katika ukanda huu timu zisipate fedha? Maana kila mechi
inapoonyeshwa ‘live’, mashabiki wengi wanaacha kwenda uwanjani.
Kitaalamu hapa
timu zinapata hasara, kama hazipewi kitu, basi lazima tukubali zitakuwa
zinatumika vibaya na kama udhamini huo Cecafa inachukua kila kitu, basi kuna
tatizo.
Klabu lazima
zikubali kwamba bila zenyewe hakutakuwa na Cecafa. Lazima viongozi wake waamke
na kuhoji kwamba SuperSport imetoa kiasi gani na zenyewe zinapata nini.
Kwani Cecafa
inashughulikia kukuza vijana? Hapana. Sasa kama inalipwa na SuperSport, fedha
zote zinakwenda wapi? Ni kulipa waamuzi na malazi ya timu? Kama ni hivyo tu,
basi tujue mkataba huo unaipa Cecafa fedha kiasi gani kila mwaka na mwisho wao
waweke wazi matumizi.
Nasema hivi
ili kusisitiza mabadiliko ya timu zetu, hasa za Tanzania kuendelea kutumiwa tu
huku wachache wakifaidika kwa faida yao. Haya lazima yawekwe wazi ili tuwe
katika ulimwengu wa uwazi.
Si rahisi
tuendelee kukubali kukaa kimya, tukionyesha uoga au nidhamu ya uoga wakati
mambo yanaendelea kudidimia. Klabu zinaingia gharama kubwa, eti kisa
zinaonekana ‘live’. Mtafakari hili, mimi naweka akiba, nitarudi tena.
0 COMMENTS:
Post a Comment