August 21, 2015


Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mchezaji wa Akademi ya Alladini iliyopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga,  Ally Jacob Madanganya, ameuawa kikatili kwa kuchomwa kisu na watu wasiojulikana na kufariki dunia papo hapo wakati akiwa njiani kuelekea mazoezini.


Tukio hilo lilitokea juzi jioni maeneo ya Majengo ambapo alikuwa akielekea mazoezini kwenye Uwanja wa Halmashauri Kahama kujumuika na wenzake katika mazoezi ya kujiandaa na mashindano ya Ligi Daraja la Nne Wilaya ya Kahama.

Kocha Mkuu wa Akademi Alladini, Imam Omary Mabrouk, alisema: “Mimi huwa nina kawaida ya kufanya mazoezi mapema, hivyo wakati tukiwa uwanjani tukiendelea na mazoezi, Ally ambaye ni mmoja wa wachezaji wangu, alipatwa na mkasa huo kwa kuvamiwa na watu wasiojulikana waliomshambulia.

“Tumesikitishwa sana na tukio hilo la Ally ambaye alikuwa ni beki muhimu kikosini kwetu, mara baada ya tukio hilo kuna mmoja wa wale waliomvamia alikamatwa na wananchi na mpaka sasa yupo chini ya ulinzi wa jeshi la polisi.

“Tunatarajia kumpumzisha mwenzetu leo (jana), mambo mengine ya uchunguzi, sababu za tukio hilo na usalama yanaendelea kufanywa na polisi.

“Ally alikuwa na miaka 17, nilizungumza na baba yake alisema wanaye walikuwa wakilalamika kufuatwafuatwa na watu wasiowajua lakini hakutilia maanani, hivyo tukio hilo limemfanya kuhisi kulikuwa na uhusiano baina ya alichoelezwa na wanaye na tukio hilo.”

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic