NILIAMUA
kusikiliza kwa umakini alichokuwa akikizungumza aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Wilbroad Slaa wakati akiwa ameibuka kwa mara ya kwanza baada ya
ukimya wa muda mrefu.
DK
Slaa alikaa kimya kwa muda mrefu kabla ya siku hizo chache zilizopita
alipoibuka na kuzungumza mengi ambayo naweza kusema hapa si mahali pake.
Wakati
akizungumza mengi, yako niliyoshika kwa maana ya kufurahishwa na namna
alivyokuwa akijieleza na hasa ile kuonyesha yuko tayari kushikilia
anachokiamini.
Dk
Slaa amezungumza mengi sana, lakini kuna alilolieleza kwamba “Acha nife,
wajukuu zangu watakapochimbua kaburi waone jina langu, watatoa hukumu sahihi.”
Hii
ilinifanya nikumbuke mengi sana kuhusiana na michezo ya Tanzania na hasa soka.
Najua kuna matatizo mengi hata kwenye netiboli, riadha, ngumi na inaonekana
michezo ndiyo kichaka cha wajanjawajanja wengi ambao wanaona huko ndiyo sehemu
sahihi ya kujificha.
Ukiona
maendeleo ya michezo katika nchi nyingi duniani, utagundua hakuna viongozi
sahihi wa soka na hasa wenye mapenzi hasa na michezo husika na wengi ni wale
wanaotaka kujiendeleza wao binafsi, au kuzifurahisha nafsi zao na si mapenzi ya
dhati ya wanachokitumikia.
Ili
kuwa na mafanikio katika kitu fulani, basi mapenzi ya dhati lazima yawepo kwani
watu wanatakiwa kufanya chochote kwa dhati na bila mapenzi, basi haitawezekana.
Nitaweka
mengi kwa jumla nikianza na soka, angalia namna Yanga na Simba zinavyoishi
maisha ya kubahatisha licha ya ukubwa wao kwa kwa maana ya mtaji mkubwa wa jina
na wingi wa watu.
Yanga
na Simba, hazina hata uwanja wa kufanyia mazoezi, kitu ambacho unaona ni sehemu
ya maajabu ya soka kwamba hivi ni kweli viongozi wa Yanga na Simba hawaoni kama
timu zao zinahitaji uwanja wa mazoezi?
Kweli
unaweza ukaniambia Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji na Rais wa Simba, Evans
Aveva hawajui timu zao zinahitaji viwanja na hawajui umuhimu wake? Jibu
litakuwa wanajua, lakini vipi hawalifanyii kazi kwa muda wote waliokuwepo hapo.
Si
uwanja wa mechi, nazungumzia uwanja wa mazoezi tu. Unafikiri viongozi hao na
wengine wa kamati za utendaji hawajui? Ndiyo maana ninarudia ile kauli ya Dk
Slaa ya hukumu ya wajukuu zake.
Kweli
Aveva na Manji wamewahi kuwaza hivyo kwamba siku moja wataingia kwenye hukumu
ya moja ya viongozi wakubwa wa soka walioongoza klabu kubwa na kongwe za Yanga
na Simba, lakini zikawa hazina hata viwanja vya mazoezi?
TFF
nayo imekuwa ikiingia kwenye migogoro mingi kila kukicha. Migogoro mingine kama
ule wa kufungiwa kwa Dk Damas Ndumbaro. Wazi unaonyesha ni ubinafsi, ubabe wa
kipuuzi lakini umefanyika. Je, Malinzi na wenzake hawahofii kuhukumiwa baadaye?
Anachokisema
Dk Slaa, sina uhakika na ukweli wake lakini nazungumzia kauli hiyo ambayo
kwangu inaonyesha angalau ni kiongozi anayeweza kuhofia jambo fulani la
uadilifu hadi kufikiria vizazi vijavyo vitamfikiria au kumhukumu vipi hapo
baadaye.
Nilitamani
viongozi wote wa soka, kuanzia TFF, vyama vyote, klabu kubwa kama Simba na
Yanga, ndogo na nyingine changa wawe waoga angalau wafikirie hukumu yao kesho
itakuwaje.
Wawe
waoga wa kuonekana hawakufanya lolote, wasifikirie leo pekee na wabadilike kwa
kuamini Yanga kuifunga Simba au Simba kuifunga Yanga ndiyo mafanikio makubwa.
Lazima
tukubali, viongozi wengi wa michezo ndiyo ugonjwa wa maendeleo duni ya michezo
na kama hawatabadilika na kufikiria huko mbele watahukumiwa hata na wajukuu
zao, basi milele michezo itabaki tulipo na porojo ndiyo zitashika hatamu kama
ilivyo sasa huku tukisubiri mafanikio ambayo yatabaki kuwa ndoto isiyofikiwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment