Wakati Ligi Kuu Bara ikitarajiwa kuanza Septemba
12, 2015, tayari tambo zimeanza kuwa nyingi huku Kocha wa Simba, Dylan Kerr
akijinadi kuwa amepania kuivunja rekodi ya timu yake kutoshinda kwenye Uwanja
wa Mkwakwani, Tanga.
Simba imekuwa ikipata wakati mgumu uwanjani hapo
kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita, bila kujali inacheza na timu ipi katika
ligi kuu.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo Simba itafungua
pazia uwanjani hapo kwa kukipiga na African Sports ambayo imepanda daraja hivi
karibuni, kisha itabaki Tanga kukipiga na Mgambo JKT kwenye dimba hilohilo.
Kerr amesema hana hofu juu ya uwanja huo wala
hatishwi na rekodi ya timu yake kutofanya vizuri uwanjani hapo.
“Sijawahi kucheza uwanjani hapo lakini hiyo
hainipi hofu na malengo yangu ni kuweza kuvunja hiyo rekodi mbaya ya kutofanya
vizuri kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri kwa michezo yake yote ambayo
itacheza hapo.
“Ni vizuri kuanza ligi vema kwa kuwa na matokeo
mazuri ambayo yatawapa nguvu zaidi ya kujituma na kufanya vizuri, nina
wachezaji wazuri ambao wanajua nini wanafanya, hilo nalo litanisaidia kwa kiasi
kikubwa,” alisema Kerr.
Rekodi zinaonyesha matokeo ya Simba kwenye Uwanja
wa Mkwakwani kwa misimu mitatu iliyopita yalikuwa hivi: 2012/13, Coastal Union
0-0 Simba, Mgambo 0-0 Simba. Msimu wa 2013/14, Mgambo 1-0 Simba, Coastal Union
0-0 Simba, Msimu wa 2014/15, Mgambo 2-0 Simba,
Coastal Union 0-0 Simba.
Upande wa Yanga uwanjani hapo rekodi zipo hivi:
2012/13, Coastal 0-2 Yanga. 2013/14 Mgambo 1-0 Yanga, Coastal 0-0 Yanga.
2014/15 Mgambo 0-2 Yanga, Coastal 0-1 Yanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment