Ligi Kuu Bara inaanza leo huku gumzo likiwa ni uwezo wa makocha
sita kutoka Ulaya ambao wanaandika historia ya kuzifundisha timu za ligi hiyo
kwa pamoja ndani ya msimu mmoja.
Timu sita za ligi kuu zinafundishwa na makocha
raia wa nchi za Ulaya ambao ni Hans van Der Pluijm wa Yanga raia wa Uholanzi,
Dylan Kerr (Uingereza, Simba), Stewart Hall (Uingereza, Azam FC) na Patrick
Liewig raia wa Ufaransa.
Wengine ni Martin Grelics wa Toto Africans raia
wa Ujerumani na Mika Lonnstorm wa Majimaji raia wa Finland.
Wote wameshaanza
kazi na katika vikosi vyao na leo Jumamosi watakuwa katika mitihani isipokuwa
Pluijm.
Kerr ataiongoza Simba dhidi ya African Sports
kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga, na tayari amejitamba kushinda mchezo huo
wa kwanza kwake katika ligi kuu.
“Tupo vizuri na kitu pekee tunachosubiri ni
kuingia uwanjani kutekeleza kile tulichojifunza kwa muda wote,” alisema Kerr
ambaye anasifika kwa soka la kasi na la pasi fupifupi.
Hall yeye ataiongoza Azam katika mchezo dhidi ya
Prisons kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam ambapo
ametamba kufanya vizuri huku akitumia rekodi ya kuchukua ubingwa wa Kombe la
Kagame bila kufungwa hivi karibuni.
“Tunahitaji kujituma ili kuweza kushinda mchezo
huu, naamini mchezo utakuwa mgumu na wa kiushindani, lakini kwa upande wa
wachezaji wangu safu zote zipo imara,” alisema Hall.
Grelics wa Toto na Lonnstorm wa Majimaji wenyewe
hawakuwa na maneno mengi zaidi ya kusema wanasubiri kucheza mechi za kwanza ili
kujua ligi ilivyo na baada ya hapo wanaweza kuwa na mwanga na ligi ya Tanzania.
Toto itacheza na Mwadui FC nyumbani CCM Kirumba
wakati Majimaji itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Majimaji kucheza na JKT Ruvu.
Kocha wa zamani wa Simba, Liewig atakuwa
nyumbani CCM Kambarage akiiongoza Stand United dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mzungu mwingine ambaye ni bingwa mtetezi, Pluijm
kesho Jumapili ataiongoza Yanga dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
“Mechi ya kwanza siku zote inakuwa na ‘tension’
kubwa, hasa kwa wachezaji na mashabiki, lakini kama unavyojua siku zote sisi,
tunahitaji kupata pointi zote na kusonga mbele zaidi,” alisema Pluijm.
Katika mechi nyingine za leo, Ndanda FC itakuwa
nyumbani kucheza na Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Mbeya City itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.







0 COMMENTS:
Post a Comment